Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
CHUO cha ualimu, Ushirika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, kimesambaza
wanachuo kutoka katika chuo hicho kwenda shule mbalimbali za msingi wilayani
humo, ili waweze kuanza mazoezi ya kufundisha watoto shuleni.
Mwandishi wetu akizungumza na Mkuu wa chuo hicho, Awadh
Nchimbi alisema kuwa tayari wanachuo 120 wamekwisha pelekwa katika shule hizo,
wakiwemo wanaume 80 na wanawake 40.
Alifafanua kuwa, chuo kimedhamiria kufanya hivyo ili kuweza
kujenga misingi imara ya kuwajengea uwezo wa kufundisha wanachuo hao pale
wanapokuwa darasani, ili baadaye watakapohitimu masomo yao waweze kufanya vyema
kwa vitendo na kufuata weledi wa kazi ya ualimu.
Nchimbi aliongeza kuwa kutokana na uhaba wa majengo
waliyonayo chuoni hapo, pia wanampango wa kuhakikisha kuanzia sasa wanajenga
majengo ya kutosha hususani, mabweni ya kulala wanafunzi ili kuweza kukidhi
mahitaji husika kutokana na yaliyopo sasa kutojitosheleza.
Aidha imeelezwa kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho,
kunahamasisha wazazi wenye watoto kusomesha kwa bidii wakiwa na lengo la
kuwataka kujiunga na chuo cha ualimu, Ushirika baada ya kuona vijana kutoka
maeneo mbalimbali mkoani humo, kwenda kujiunga na masomo ya ualimu.
Pamoja na mambo mengine, chuo hicho kipo katika kijiji cha
Nahoro kata ya Luegu wilaya ya Namtumbo, Ruvuma umbali wa kilometa 10 kutoka
makao makuu ya wilaya hiyo, kuelekea Songea mjini.
No comments:
Post a Comment