Na Mwandishi wetu,
NIMECHUKUA jukumu la kuvishauri vyama vya wafanyakazi pamoja
na shirikisho la wafanyakazi hapa nchini, kutokana na hali halisi ya utatanishi
kati ya waajiri na wafanyakazi katika mahusiano yao. Mahusiano hasi kati ya
mwajiri na mwajiriwa yamekuwa nikawaida katika mazingira ya kazi hapa nchini.
Binafsi naamini vyama vya wafanyakazi ni kiungo kati ya
waajiri na wafanyakazi hivyo kuwa daraja katika kushughulikia kero, changamoto
au matatizo mbalimbali kati ya mwajiri na mfanyakazi, pia hushughulikia kutoa
msaada wa kisheria kwa inapobidi.
Licha ya hapa kwetu Tanzania, kuwa na vyama vya wafanyakazi
pamoja na juhudi mbalimbali za vyama hivyo bado kumekuwa na changamoto nyingi
zinazowakabili wafanyakazi.
Hivyo upo umuhimu wa vyama hivyo kushirikiana na taasisi
binafsi kutoa msaada wa kisheria pamoja na elimu kwa wafanyakazi, ili kuondoa
hali ya manyanyaso, ukiritimba na urasimu unaofanywa na waajiri kazini.
Leo hii tunaelekea Mei mosi, maadhimisho ya wafanyakazi wote nchini,
je ni lipi la kujivunia sisi kama wafanyakazi? je kama wafanyakazi tumeweza
kupata mafanikio kutokana na changamoto zile zilizotukumba kabla ya Mei mosi ya
2014? je ipi ni taswira ya vyama au mashirikisho ya vyama vya wafanyakazi? je
wafanyakazi wana taswira chanya au hasi dhidi ya vyama au shirikisho la
wafanyakazi? je kwa nini wanamtazamo chanya au hasi dhidi ya vyama au
shirikisho la wafanyakazi?
Najua changamoto kubwa itakuwa ni wafanyakazi wengi kutokuwa
tayari kujiunga na vyama vya wafanyakazi, kuchangia ada zao au kuwa tayari
kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwa kujaza fomu namba TF6 kwa ajili ya kuhudhuria
nakukubaliana na vyama vya wafanyakazi? je kwa muda huu wa mwaka mmoja toka
tuadhimishe sikukuu ya wafanyakazi tumepiga hatua au tumerudi nyuma?
Je vyama vimetoa elimu kwa wanachama au wafanyakazi wao, juu
ya wajibu na stahiki zao muhimu? je ni kwa kiasi gani vyama vimeweza kutoa
msaada wa kisheria kwa wanachama wao? je ni kwa namna gani vyama vimekuwa na
ushawishi ambao umesaidia wanachama wao kujiunga kwa hiari, ili kuweza kupanua
wigo wa kuwasaidia wafanyakazi wengi zaidi?
Je ni kwa namna gani vyama vya wafanyakazi, vimeweza kutatua
migogoro ya kazi bila kuathiri shughuli za mwajiri? je ni kwa namna gani vyama hivyo
vimeweza kuwadhibiti waajiri wanaoenda kinyume na taratibu au kanuni za
mahusiano kazini kati ya mwajiri na mfanyakazi?
Haya ni maswali yangu tu machache lakini, nitatolea mifano
kadha wa kadha inayoweza ikasaidia kuonyesha ni kitu gani kinatakiwa kifanyike,
ili kunusuru hali ya wafanyakazi hasa wanaoajiriwa kiholela bila mikataba wala
mfumo rasmi wa malipo, hii inatokana na uzoefu wangu nilioweza kuupata kwa muda
mfupi baada tu, ya kujihusisha kupigania haki stahiki za wafanyakazi.
Nimekuwa nikifuatilia ajira za walinzi binafsi, katika sekta
binafsi na zile za umma mfano masokoni, maduka, shule na hata ofisi za umma,
pia ajira za upishi katika shule za msingi na sekondari naamini hizi zote ni ajira
ambazo zinatakiwa kuheshimiwa, na wapo kwa ajili ya kuwasaidia waajiri ili
waweze kutimiza adhma yako kutokana na malengo yao binafsi au ya taasisi
husika.
Pia zipo ajira zinazotolewa kwenye sehemu za starehe maarufu
kama bar, grosary, mahotelini nakadhalika nao kwa upande wao kunachangamoto
nyingi hasa dhidi ya ukatili wa wanawake, kudhalilishwa na kunyanyaswa nako
huku tunasikia vipo vyama vinavyowatetea. Pia hata wale wafanyakazi wanaofanya
kazi majumbani (House boy na House girl) nao wanachangamoto nyingi je nani
anawajali?
Haya yote yanatokea ikiwa tuna serikali inayotoa miongozo
kila mwaka, chini ya Wizara ya kazi ajira na vijana juu ya viwango vya
mishahara kwa sekta binafsi na umma, lakini mwisho wake hayupo mtu au taasisi
binafsi inayowalipa walinzi, wapishi, wafanyakazi kwenye sehemu za starehe, mahouse
girl na house boy?
Nani awasaidie wafanyakazi hawa wajue stahiki zao, au nani awasaidie
kutatua migogoro kati yao na waajiri wao ikiwa tu kila wanapodai stahiki zao
wanaishia kubambikizwa kesi, kupigwa na hata wengine kufukuzwa kazi lakini
vyama vya wafanyakazi vimebakia kuwa na ofisi mijini tu.
Kundi hili utakuta linapewa ajira bila mikataba, hivyo hata inapofikia
muda utakuta kuna migogoro, wakati huo wafanyakazi hawa hawana pa kusimamia na
chakuumiza zaidi hawana elimu yoyote ile ya haki na wajibu wa mfanyakazi, elimu
dhidi ya viwango vya ujira kwa kazi zao, je nani awasaidie?
Ni imani yangu mfanyakazi akiwa ametimiza wajibu wake
inatakiwa apewe stahiki sahihi hivyo, nashauri ni vyema waajiri wakaliona hilo
na pia vyama vya wafanyakazi vione haja ya kuwasaidia wafanyakazi, ambao ndio
wanachama wao kwa kuwapatia taarifa sahihi ikiwa pamoja na haki stahiki,
nyaraka maalum za malipo na pia ikiwa pamoja na msaada wa kisheria pale
inapobidi.
Ushauri wangu, itakuwa ni kichekesho kwa vyama vya
wafanyakazi kuishia kuadhimisha maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei
Mosi) huku wafanyakazi wake wakiwa wanaishi maisha duni, yenye manyanyaso,
dhuluma na chuki. Pia itakuwa ni kichekesho kwa vyama vya wafanyakazi nchini, vikiwa
na taswira hasi dhidi ya wanachama wao maana utakuwa ni mwanya kwa waajiri
kuendelea kuwakandamiza wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment