Na Stephano Mango,
Songea.
HALMASHAURI ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, imetoa shilingi
milioni 259.5 kwa ajili ya utekelezaji ujenzi wa maabara, kwa shule za sekondari
23 ambazo zipo katika halmashauri hiyo, ili kuweza kukamilisha zoezi la ujenzi
wa miundombinu yake.
Akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika
hivi karibuni mjini hapa Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Sigsiberth Valentine
alisema halmashauri inaendelea kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete, ujenzi
wa maabara tatu kwenye kila shule ya
Sekondari wilayani humo.
Valentine alisema, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba
mwaka jana, halmashauri yake ilikwishatoa fedha na vifaa vya viwandani, vyenye
thamani ya shilingi milioni 259,582,239 kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema kuwa fedha hizo zimetumika kuwalipa mafundi na
ununuzi wa vifaa hivyo, na kwamba kilichobaki sasa asilimia kubwa ni ujenzi wa
miundombinu ya vyumba vya maandalizi (Preparation rooms) katika maabara hizo,
kufunga mitungi ya gesi na kupaka rangi majengo hayo.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa sekondari zingine zipo kwenye
hatua ya mwisho wa ujenzi, na taratibu za kukamilika zinaendelea kwa kasi ili
kuweza kufikia lengo husika.
Alizitaja shule ambazo zinajengwa maabara hizo katika wilaya
ya Songea kuwa ni; Nguruma, Maposeni, Nalima, Magingo, Lipupuma na Gumbiro
ikiwa zote ni za kata.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Rajabu Mtiula
aliwataka wakuu wake wa idara kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati, wasimamie
vyema rasilimali zote zinazotolewa na serikali, ili kuweza kukamilisha kazi
hiyo ipasavyo na kwa viwango vinavyokubalika.
Mtiula alisema kila mkuu wa idara anapaswa kutumia nguvu zake
zote kuhakikisha ujenzi huo unafanikiwa, kwani licha ya kuwa ni agizo la Rais
lakini ni muhimu kwa faida ya kizazi hiki cha sasa, kijacho na taifa kwa
ujumla.
No comments:
Post a Comment