Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
MADIWANI wa Hamashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,
wamepitisha bajeti ya halmashauri hiyo, bila mabadiliko na makadirio ya mapato
na matumizi kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ya shilingi bilioni 49.4.
Halmashauri hiyo ilifikia maamuzi hayo katika kikao
maalum cha baraza la madiwani ambacho ni cha bajeti, ukumbi wa Klasta ya walimu
mlingoti, mjini hapa.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo, fedha hizo kati yake shilingi
bilioni 37.3 zitatumika kulipa mishahara, bilioni 2.7 ni kwa ajili ya matumizi
mengineyo na bilioni 6.4 ni fedha za miradi ya maendeleo, zote zikiwa
zinatokana na ruzuku kutoka serikali kuu pamoja na wadau wa maendeleo.
Aidha halmashauri hiyo inatarajia kukusanya shilingi bilioni
2.6 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani.
Akifafanua bajeti hiyo Mratibu wa rasimu ya mpango wa bajeti
ya mwaka 2015/2016, afisa mipango wa halmashauri ya wilaya hiyo, Frednand
Filimbi alisema kuwa kupitia mpango wa bajeti hiyo, halmashauri yake imepanga kukusanya
na kutumia jumla ya shilingi bilioni 49.438,553,315 katika kipindi cha
mwaka huo wa fedha.
Kadhalika aliwahimiza madiwani katika halmashauri yake
kuongeza nguvu katika uhamasishaji wa wananchi wao, kujitolea katika utekeleza
wa miradi kwenye maeneo yao.
Filimbi aliendelea kufafanua kuwa taarifa za mapitio ya
bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015 hadi kufikia mwezi Disemba, halmashauri
ilipokea chini ya asilimia 50 ya bajeti yake, hali ambayo alisema kuwa imeathiri
utekelezaji wa miradi yao.
Wakichangia kwa nyakati tofati, diwani wa kata ya Mlingoti
Magharibi Mchemela Abdalah (CUF), Kitumbi Hamadi wa kata ya Mchesi (CCM) na diwani
wa kata ya Marumba Msenga Said (CCM) waliilalamikia serikali kuu, kwamba kitendo
cha kutopeleka fedha hizo za ruzuku katika halmashauri yao kwa wakati, kimekuwa
chanzo cha kutotekelezeka kwa miradi ya maendeleo ya wananchi katika
halmashauri hiyo.
Katika taarifa zao madiwani hao walizungumzia pia, kukwama
kwa ujenzi wa miradi ya ofisi za kata ya mlingoti magharibi ambayo ilipangiwa
bajeti yake, lakini baada ya kukosekana kwa fedha hizo mradi huo, ulionekana
kutotambuliwa na kunyimwa fedha katika bajeti ya mwaka 2014/2015 hali
aliyopelekea malalamiko kutoka kwa wananchi.
Madiwani hao walisikitishwa na taarifa za kutokuwepo kwa
bajeti ya ujenzi wa madarasa katika shule za msingi, ikiwemo shule ya Msinjili
ambayo mwaka 2014 ilipata maafa ya kubomokewa kwa madarasa yake, kutokana na kunyesha
mvua ambayo iliambatana na upepo.
Kufuatia hali hiyo diwani wa kata ya Ligunga (CHADEMA)
Kazembe Said, akaja na hoja ya kuwataka watendaji kutekeleza wajibu wao
ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kutekeleza ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na
viongozi wa serikali.
Kazembe alitolea mfano wa ahadi zilizosahaulika kuwa mwaka
2005 waliokuwa wakuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Kalembo na Monica Mbega waliahidi wananchi
wa kijiji cha Mtangashari kuwa, watajengewa zahanati lakini hadi sasa hakuna
kilichotekelezwa.
Awali katika ufunguzi wa kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri
ya wilaya ya Tunduru Faridu Khamisi aliwataka wajumbe wa kikao hicho kuipitia
kwa makini bajeti hiyo, na kutoa michango yao kwa uwazi itakayosaidia
kuiboresha na kutoa miongozo na maelekezo yaliyozingatiwa, wakati wa
kukamilisha maandalizi ya mwisho kabla haijafikishwa katika ngazi za juu kwa
ajili ya utekelezaji.
No comments:
Post a Comment