Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa makini na kufuatilia juu ya mfumo wa matumizi, mashine za kisasa (BVR) kwenye ukumbi wa Chuo cha maendeleo Mbinga mjini. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
TUME ya Taifa ya uchaguzi hapa nchini, imeendesha mafunzo kwa
Waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, juu ya
mfumo wa matumizi, mashine za kisasa (BVR) ambazo zitatumika kwa ajili ya
uandikishaji wapiga kura, katika daftari la kudumu mapema mwaka huu.
Mafunzo hayo ambayo yameendeshwa kwa siku mbili, katika
ukumbi wa chuo cha maendeleo ya jamii wilayani humo, yanalenga uboreshaji wa
daftari hilo kwa lengo la kudhibiti mianya ya udanganyifu kwa baadhi ya watu,
ambao hujiandikisha zaidi ya mara moja.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Afisa uchaguzi
kutoka makao makuu ya tume hiyo, Crecencia Mayalla alisema mfumo huo
unarahisisha pia utendaji kazi wakati wa zoezi hilo la uandikishaji wapiga
kura, ambalo linatarajiwa kuanza hivi karibuni.
“Mashine hizi zinatengeneza kadi ya mpiga kura, ambayo
inamwezesha mtu kufungua akaunti benki, kumdhamini polisi, kupata paspoti ya
kusafiria na hata cheti cha kuzaliwa”, alisema Mayalla.
Awali akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi
Ngaga aliwataka washiriki kuzingatia taaluma waliyoipata na kuwa waangalifu juu
ya matumizi ya mashine hizo, kutokana na umuhimu wa zoezi hilo katika jamii.
Mkuu huyo wa wilaya, aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo
kuwa waangalifu wakati wa matumizi wa mashine hizo, ili zisiharibiwe kwa kuwa
serikali imezinunua kwa gharama kubwa.
Ngaga alisema, kwa mwandikishaji ambaye ataona hawezi kumudu
namna ya kutumia mashine hizo, ni vyema akajiondoa mapema ili asiweze kuharibu
mwenendo wa zoezi hilo.
“Napenda kutoa wito kwenu na wananchi kwa ujumla, wakati
zoezi hili la uandikishaji litakapoanza washawishini wananchi wajitokeze kwa
wingi, na huko muendako nendeni mkawahamasishe pia waweze kushiriki kikamilifu”,
alisema Ngaga.
Hata hivyo, mmoja kati ya wakufunzi wa mafunzo hayo, Peter
Mdaki alisema kuwa, washiriki wamekuwa wepesi kuelewa juu ya matumizi ya
mashine hizo kutokana na wengi wao, kuwa na elimu ya matumizi ya kompyuta.
1 comment:
thanks for good news.........!!!!
Post a Comment