Waziri MKuu, Mizengo Pinda. |
Na
Mwandishi wetu,
Songea.
WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda amesema amevutiwa sana na kazi iliyofanywa katika muda
mfupi kwenye shamba la kahawa la Aviv, lililopo kwenye kijiji cha Lipokela,
wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma.
Alisema
katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba, eneo kubwa la shamba hilo limepandwa
miche ya kahawa na mingine imezaa na imeshavunwa, ikilinganishwa na wakati
alipofika shambani hapo Julai 2013 na kutembelea tu kitalu cha miche ya zao
hilo.
Hayo
aliyasema jana, wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi na menejimenti ya
shamba la Aviv, baada ya kutembelea na kukagua miundombuinu ya umwagiliaji wa
matone ya maji kwenye shamba hilo.
“Mkuu
wa shamba hili, Bw. Medu amenieleza kwamba mpaka sasa wameshavuna kahawa mara
moja na wanatarajia kuvuna tena hivi karibuni, lakini ili waweze kuanza kupata
faida ni lazima wavune mara nne,
“Ndugu
zangu kilimo kinataka uvumilivu na kinataka uwekezaji mkubwa.........hata kwa
wakulima wadogo ni lazima kiwepo licha ya ugumu wake. Sasa ukisema kilimo ni
kigumu na ukaacha kulima wakati una mke na watoto, je hao watakula wapi?”,
alihoji.
Aliwasifu
wamiliki wa shamba hilo kwa kuchagua kulima zao la kahawa kwani lina walaji
kila mahali ulimwenguni kote.
“Wameamua
kulima kahawa aina ya Arabica ambayo inakubalika duniani, mahitaji ya kahawa
hii yapo kila mahali kwa sababu wanywaji wapo”, alisema.
Waziri
Mkuu alisema pamoja na mafanikio hayo, shamba la Aviv linakabiliwa na
changamoto ya nishati kwani linahitaji megawati 2.5 ili liweze kuendesha
mitambo yake ambayo kwa sasa, inatumia mafuta yanayoligharimu fedha nyingi.
Aliwataka
wamiliki wa shamba hilo waendelee kuwa wavumilivu, wakati Serikali ikiendelea
kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Mapema,
akisoma risala ya kampuni ya Aviv, Mkuu wa shamba hilo ambaye pia anasimamia
uzalishaji wa zao la kahawa Afrika Mashariki, Medu Medappa alisema hadi sasa
wamekwishalima hekta 1,060 na zote zimekwishawekewa miundombinu ya umwagiliaji
wa matone na kati ya hizo, hekta 810 zimekwishapandwa miche ya kahawa.
“Shamba
letu lina ukubwa wa hekta 2,000 na hadi sasa tumeshalima hekta 1,060 na
zilizobakia ni kwa ajili ya kutunza mazingira na uoto wa asili kwenye vilima
vinavyotuzunguka,” alisema.
Alisema
hadi sasa wamekwisha ajiri wafanyakazi 1,500 kwenye shamba hilo na kutoa
mafunzo kwa wakulima wanaoishi vijiji vya jirani na kuwapatia miche bure kaya
673 kutokana na mafunzo waliyoyapata, wanavijiji wameweza pia kulima kahawa
inayoendana na viwango vya kimataifa vya uzalishaji kahawa ambavyo ni miezi 22.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akijibu moja ya hoja kwenye risala ya
Bw. Medappa iliyohusu eneo la hekta tisa kuchukuliwa na Wakala wa Ujenzi wa
Barabara (TANROADS) alisema eneo hilo ni muhimu kwa ujenzi wa barabara za mkoa
huo, kama ambavyo shamba hilo ni muhimu kwa mkoa huo.
“Lile
eneo limetengwa na TANROADS kwa ajili ya kutengeneza kokoto za ujenzi wa barabara,
barabara za lami tunazitaka tunahitaji kazi hii iendelee la sivyo barabara zetu
zitakufa”, alisema.
Alisema
watu wa TANROADS wakimaliza kazi yao, lile eneo litabaki tupu na mwekezaji huyo
anaweza kulitumia kadri atakavyoona inafaa kwa sababu liko ndani ya eneo lake.
No comments:
Post a Comment