Na Nathan Mtega,
Songea.
IMEELEZWA kuwa viongozi wa ngazi mbalimbali nchini,
wametakiwa kujipima katika utendaji wao wa kuwatumikia wananchi pamoja na wanaowaongoza
kama wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, kwa uadilifu na moyo wa uzalendo katika
taifa hili kama walivyofanya wa asisi wetu akiwemo, Hayati Rashid Mfaume
Kawawa.
Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko alisema
hayo wakati alipokuwa akifungua tamasha la kumuenzi Hayati Rashid Kawawa
linaloenda sambamba na kuwakumbuka mashujaa wa vita ya Maji maji, yanayofanyika
mjini Songea mkoa humo ambayo yameanza kwa wajumbe wa kamati hiyo ya maandalizi
inayofanya kazi chini ya Mwenyekiti wake, Fredrick Mwakalebela kwa kutembelea
baadhi ya maeneo ambayo muasisi huyo aliishi na kufanya kazi mkoani hapa.
Alisema ni vyema wakati taifa linawakumbuka viongozi na waasisi
wake pamoja na mashujaa wa vita hiyo, ambayo ndiyo ilikuwa chachu ya ukombozi
wa bara la Afrika kila mmoja kwa nafasi yake katika jamii ajitafakari kama
anatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, utawala bora pamoja na moyo wa
uzalendo kama walivyokuwa waasisi wa taifa hili, ambao huenziwa kila mwaka.
Bendeyeko alisema ili tamasha hilo na maadhimisho ya kumbukumbu
ya kuwaenzi mashujaa hao, yaweze kuwa na tija ni muhimu kwa kila mmoja
kuhakikisha anaguswa na moyo wa uzalendo waliokuwa nao waasisi hao pamoja na
mashujaa hao.
Alifafanua kuwa Hayati Rashid Kawawa, alikuwa na moyo wa
kujitoa kama walivyojitoa mashujaa wa vita ya Majimaji ambayo ndiyo ilikuwa
chachu ya ukombozi wa taifa letu na bara la Afrika huku kila mmoja anapaswa
kujionja katika uongozi wa serikali na sekta binafsi, anajitoa kwa kiasi gani
kwa ajili ya kutetea taifa na kujiepusha na ubinafsi usio na tija kwa jamii
anayoiongoza.
Kama mashujaa wa vita hivyo pamoja na waasisi wake akiwemo Hayati
Rashid Kawawa aliyejulikana pia kama simba wa vita, wasingekuwa na moyo wa
kujitoa leo kiizazi kilichopo kisingeweza kufaidi matunda ya kujitoa kwao na
taifa lingekuwa katika hali mbaya.
Awali naye mkurugenzi mkuu wa makumbusho hayo, Profesa Mabula
alisema lengo lake ni kujenga makumbusho ya kuwaenzi viongozi wa kitaifa,
katika sehemu moja ili kuendelea kudumisha historia yao kwa kizazi kilichopo na
kijacho.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni; miaka mia moja na kumi ya vita vya
maji maji na simba wa vita Rashid Mfaume Kawawa mzalendo wa kweli.
No comments:
Post a Comment