Na Kassian Nyandindi,
Songea.
SISTA Innocensia Kisaka (33) wa kanisa Katoliki, Jimbo la
Iringa mkoani Iringa amefariki dunia na wenzake sita kujeruhiwa vibaya baada ya
gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na gari jingine, ambalo
lilikuwa mbele yao katika kijiji cha Sanangura, Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma.
Ajali hiyo ilitokea kwenye barabara ya kutoka Njombe kwenda
Songea, ambapo Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema tukio
hilo lilitokea Februari 20 mwaka huu majira ya usiku, huku akimtaja aliyefariki
dunia kuwa ni Sista huyo wa kanisa Katoliki.
Kadhalika Msikhela aliwataja waliojeruhiwa ambao hivi sasa,
wamelazwa katika Hospitali ya misheni Peramiho mkoani humo kuwa ni; Padre
Jastine Sapila (70), Sista Christine Banda (63) Sista Karomere Mfuse (48)
Erasto (20) Karo Mhagama (21) na Thadei Charles (20) wote wakazi wa Seminari
kuu Peramiho.
Alifafanua kuwa siku hiyo ya tukio gari lenye namba za
usajili T 94 DDC aina ya Land Cruiser, ambalo ilikuwa linaendeshwa na Fadher
Kastori Goriama (52) wa Seminari kuu Peramiho, lilikuwa linatoka Iringa kwenda
Peramiho na kwamba liligongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T 926
CDB aina ya Suzuki Carry, lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye jina
lake halikuweza kufahamika mara moja baada ya kukimbia kusikojulikana, mara
baada ya ajali hiyo kutokea.
Baada ya magari hayo kugongana, majeruhi hao walikimbizwa
katika hospital hiyo kwa ajili ya matibabu zaidi, na kwamba hali zao
zinaendelea vizuri na chanzo cha ajali hiyo kinaendelea kuchunguzwa ikiwemo
polisi, wanamsaka dereva aliyekimbia ili hatua za kisheria ziweze kuchukua
mkondo wake.
No comments:
Post a Comment