Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda. |
Mbinga.
EMMANUEL Kapinga, ambaye ni Ofisa utumishi wa Halmashauri ya
wilaya Mbinga mkoani Ruvuma, analalamikiwa na baadhi ya watumishi wenzake wa kada
mbalimbali katika halmashauri hiyo wakidai kwamba, amekuwa akiwatolea lugha mbaya zenye kukatisha tamaa na
kutowasikiliza pale wanapopeleka hoja au matatizo yao ya msingi, ili yaweze
kufanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa muda
mrefu sasa, umebaini hata taratibu za maboresho kwa mfanyakazi, kama vile
kupandishwa cheo au kwenda masomoni, imekuwa ni tatizo kwa Ofisa utumishi huyo
kuyapitisha kwa wakati, jambo ambalo ndio maana analalamikiwa.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, vilifafanua kwa
nyakati tofauti kuwa mnamo mwezi Julai mwaka jana serikali iliweka utaratibu
kwamba, watumishi wote wenye daraja la TGS A wanafuta daraja hilo, na badala
yake wapandishwe vyeo kufikia TGS B lakini katika halmashauri ya wilaya hiyo,
Kapinga analalamikiwa akidaiwa kutolifanyia kazi jambo hilo ipasavyo kwa
kuwapandisha vyeo baadhi ya watumishi wenzake, na kufanya kuwepo na malalamiko
yasiyokuwa na msingi.
“Baadhi ya watumishi mpaka sasa hatujapandishwa vyeo wala
mishahara, licha ya serikali kuagiza jambo hili lifanyiwe kazi haraka, tokea
mwezi Julai mwaka jana”, walisema.
Aidha Mkuu huyo wa idara ya utumishi wilayani humo,
ananyoshewa kidole kuwa mtumishi ambaye anaomba kuingizwa kwenye mpango kwa
ajili ya kwenda masomoni, kwa lengo la kujiendeleza cheo alichonacho napo
imekuwa ni tatizo kufanyiwa utekelezaji husika na kuishia kupewa lugha
zisizoridhisha.
Vilevile Kapinga, amekuwa akishutumiwa kufanya mchezo mchafu
wa kunyofoa nyaraka muhimu ya mtumishi ambaye amekubaliwa na kuingizwa kwenye
mpango wa kusomeshwa na serikali, na kulazimisha asaini mkataba binafsi wa kwenda
kujisomesha mtumishi mwenyewe na sio serikali.
Habari zinaeleza kuwa, kitendo hicho kinachofanywa na mtumishi
huyo ambaye serikali ilimuamini na kumpatia idara nyeti kama hiyo, kwa ajili ya
kuweza kufafanua sera za utumishi wa umma kwa watumishi wenzake wa kada
mbalimbali ndani ya halmashauri, ni cha ubabe ambao haupaswi kuvumiliwa hivyo
achukuliwe hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama
hiyo.
Walidai kuwa hata kwa wale ambao wanadai fedha zao za uhamisho
tokea mwaka 2011 mpaka sasa, hawajalipwa madai yao na kubaki wanazungushwa bila
kupewa majibu yanayojitosheleza.
Kadhalika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
wilayani Mbinga, taarifa za uhakika zilizotufikia mezani kwetu imepelekewa malalamiko
kama hayo na kutoa majibu yanayochelea kwamba, itayafanyia kazi huku ikijua
fika halmashauri hiyo, kumekuwa na uozo wa mambo mengi ambayo inabidi yafanyiwe
kazi kwa haraka na kuweza kuleta haki sawa katika jamii.
Ditram Mhoma ambaye ni Kamanda wa TAKUKURU wa wilaya hiyo,
amekuwa akitoa majibu kwa waandishi wa habari mara kwa mara kwamba, ofisi yake
inafanyia kazi lalamiko lolote la msingi linaloletwa na mwananchi yeyote na
uchunguzi unapokamilika hatua za kisheria huchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.
Ofisa utumishi wa wilaya ya Mbinga, Kapinga alipozungumza na
mwandishi wetu juu ya tuhuma hizo ofisini kwake alikataa kuzungumzia malalamiko
hayo na kumwambia; “nenda kwanza kwa Mkurugenzi ukapate kibali cha kuzungumza nami
akikuruhusu nipo tayari kutoa ufafanuzi wa jambo lolote”.
Mwandishi wetu alipochukua hatua ya kwenda kumwona Mkurugenzi
mtendaji wa wilaya hiyo, ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo, Oscar Yapesa
alitoa ushirikiano na kuruhusu kwenda kuzungumza naye ambapo Kapinga
alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo, alikana na kusema kuwa hakuna
ukweli juu ya mambo hayo.
No comments:
Post a Comment