Watuhumiwa wanaodaiwa kuunda kikundi cha ugaidi, wakipandishwa katika karandinga la Polisi mjini Songea, mkoani Ruvuma. |
Songea.
WATU saba wanaodaiwa kuunda mtandao wa kigaidi katika
Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma wamekamatwa mkoani humo, na watafikishwa Mahakamani
wakati wowote, kujibu mashtaka yanayowakabili.
Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa watuhumiwa
hao ambao majina yao yamehifadhiwa, wanatuhumiwa kuhusika na matukio matatu
tofauti ya urushaji na utegaji wa mabomu ya kienyeji mkoani humo.
Msikhela alisema, tukio la kwanza lilitokea Septemba 16 mwaka
jana, majira ya saa 1.30 jioni huko katika eneo la Misufini mjini Songea,
ambapo kikundi hicho kinachojihusisha na ugaidi huo kiliwarushia askari polisi
waliokuwa doria siku hiyo, bomu la kienyeji ambalo lilisababisha askari watatu
kujeruhiwa vibaya.
Katika tukio lingine ambalo lilitokea Oktoba 27 mwaka jana,
majira ya saa 10 jioni bomu lilichimbiwa ardhini katika eneo la Mshangano, katika
eneo ambalo hutumiwa kama kituo cha ukaguzi wa magari yanayotoka na kuingia
Songea mjini na askari wa kikosi cha usalama barabarani, kando kando mwa barabara
inayotoka Songea kwenda Njombe kwa lengo la kuwalipua askari wa kikosi hicho.
Kamanda huyo alieleza kuwa kabla hawajatimiza azma hiyo,
askari hao wa usalama barabarani waliokuwa kwenye eneo hilo, waligundua bomu
hilo likiwa limechimbiwa ardhini na kwamba jeshi la polisi mkoani humo, kwa
kushirikiana na Jeshi la Wananchi (JWTZ) baada ya kupata taarifa hiyo, walifika
eneo la tukio na kuweza kulitegua kabla ya kuleta madhara.
Aidha Msikhela alitaja tukio lingine la tatu kuwa lilitokea
Disemba 25 mwaka jana, majira ya 1.30 usiku katika eneo la Majengo Kotazi mjini
hapa, ambapo kikundi hicho cha ugaidi kiliwarushia bomu askari waliokuwa
wanafanya doria siku hiyo na mtu mmoja kutoka katika kikundi hicho, alipojaribu
kuwarushia bomu askari hao, kabla ya kurusha lilimlipukia yeye mwenyewe na
kufariki dunia papo hapo na kusababisha askari wawili kujeruhiwa.
Timu ya upelelezi toka ndani ya jeshi la Polisi, kwa kushirikiana
na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vimeweza kubaini eneo linalotumika kwa
mafunzo ya kigaidi na kikundi hicho, hivyo mpaka sasa watu saba wanashikiliwa
na jeshi hilo na wanatarajia kupanda kizimbani wakati wowote kuanzia sasa.
No comments:
Post a Comment