Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Hawa Ghasia.
|
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
KWA nyakati tofauti baadhi ya watumishi ambao ni Watendaji wa vijiji na kata, wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameendelea kumshutumu Ofisa utumishi wa Halmashauri ya
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Emmanuel Kapinga kuwa amekuwa akifanya
upendeleo wakati wa upandishaji vyeo kwa watumishi wa kada hizo, jambo ambalo wamedai
kuwa kwa namna moja au nyingine, huenda kuna mkono mchafu wa rushwa.
Aidha wameiomba Taasisi ya Kuzuia, Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) na vyombo vingine vinavyotetea watumishi kazini, kufanya upembuzi
yakinifu ikiwemo kuchunguza mwenendo wa utendaji kazi wa Ofisa huyo, ili
kuondoa matatizo yanayoendelea kujitokeza mara kwa mara katika ofisi hiyo na ambayo
yanawafanya wakose haki zao za msingi.
Mwandishi wetu, amebaini pia hata utekelezaji wa Waraka wa
maendeleo ya utumishi namba moja wa mwaka 2013 ambao unawataka watendaji wakuu
katika halmashauri nchini, kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuwapandisha
vyeo watumishi wa kada hizo, amekuwa hatekelezi kwa wakati huku agizo hilo tangu
lilipotolewa na Ofisi ya Rais, chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ndio
maana leo linazua malalamiko miongoni mwao.
Pia waraka ulitolewa na Menejimenti ya utumishi wa umma,
Februari 27 mwaka 2014 umeagiza na kutaka kutumika kwa miundombinu husika ya
utumishi kazini, na kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza
katika utekelezaji wake hasa kutokana na uhaba wa watumishi wenye sifa
zinazotakiwa, katika usimamizi wa rasilimali na miradi ya maendeleo katika
ngazi ya kijiji, mtaa na kata.
Aidha umekuwa ukifafanua namna ya upandishaji wa vyeo na
ngazi ya mshahara, ambapo utekelezaji wake ulianza mapema Julai Mosi mwaka 2013
huku ukiagiza watendaji wakuu wa mamlaka za serikali za mitaa wanapaswa
kushughulikia ajira, maslahi na maendeleo ya watumishi wa kada za watendaji wa
vijiji, mitaa na kata waliopo katika mamlaka zao.
Waraka huo unafuta nyaraka za maendeleo ya watumishi serikali
za mitaa namba 29,30 na 31 za mwaka 2003 zilizotolewa na Ofisi ya Rais tume ya
utumishi wa serikali za mitaa (TUMITAA) na kwamba watendaji wa vijiji, kata na
mitaa waliopo kazini ambao hawana sifa husika wataendelea kubaki katika vyeo walivyonavyo
bila kupanda daraja, hadi pale watakapojipatia sifa stahiki.
Hivyo basi, kwa watendaji wa kada hizo wilayani Mbinga,
baadhi yao ambao wana sifa ya kupanda daraja na ngazi ya mshahara wamekuwa
wakilalamika kwa muda mrefu kwamba hashughulikii ipasavyo masuala yao ya
upandishaji wa vyeo, mishahara na hata malipo ya fedha za uhamisho kwa wakati.
Kwa nyakati tofauti walidai kuwa, watakwenda kumshtaki kwenye
mamlaka za juu ili waweze kupata haki zao za msingi, ukizingatia kwamba wao ni
watumishi wa umma kama alivyo yeye hivyo wanakila sababu kupatiwa haki zao za
msingi, kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Pamoja na mambo mengine Kapinga, alipotafutwa ili aweze kuzungumzia
hilo na kutoa ufafanuzi wa kina juu ya madai hayo, hakuweza kupatikana ofisini
kwake na simu yake ilikuwa haipatikani.
No comments:
Post a Comment