Tuesday, February 3, 2015

UPEPO MKALI ULIOAMBATANA NA MVUA WAEZUA NYUMBA 53 TUNDURU


Na Steven Augustino,
Tunduru.

UPEPO mkali ambao uliambatana na mvu iliyokuwa inanyesha kwa masaa kadhaa, umesababisha nyumba 53 kuezuka na nyingine kubomoka katika kijiji cha Sisi kwa sisi, kilichopo kata ya Sisi kwa sisi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma na kuacha familia hazina makazi.

Aidha taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa, upepo huo umeezua nyuma 51 za bati na mbili zilizokuwa zimeezekwa kwa nyasi.

Kufuatia tukio hilo imebainishwa kuwa hasara iliyojitokeza ni ya zaidi ya shilingi milioni 53.925.

Taarifa za tukio hilo zinafanua kwamba, tukio hilo lilitokea January 27 mwaka huu, majira ya saa 10 jioni katika kijiji hicho na kuzuka taharuki kubwa kwa wakazi wa kijiji cha Sisi kwa sisi wilayani humo.


Sambamba na tukio hilo pia upepo huo uliangusha miti mingi midogo kwa mikubwa, ambayo pia iliangukia baadhi ya nyumba.

Akizungumza kwa njia ya simu Ofisa mtendaji wa kata hiyo, Neema komba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa, wahanga waliopatwa na mkasa huo hivi sasa wamehifadhiwa katika nyumba za majirani zao ambazo hazikuezuliwa.

Naye mwenyekiti wa kamati ya maafa, ulinzi na usalama ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho pamoja na mambo mengine alisema kuwa baada ya tukio hilo kutokea, kamati yake iliwatembelea wahanga hao na kuwapa pole.

Alisema wakiwa katika eneo hilo pia walizungumza na wahanga hao pamoja na kuwapatia ushauri wa kufuata, hatua za ujenzi imara wa nyumba zao pamoja na kupanda miti ya kujikinga na upepo mkali.  

No comments: