Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Mahela,
wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamenusurika kupoteza maisha yao kufuatia kundi
la nyuki kuwavamia na kuwauma sehemu mbalimbali za miili yao, wakati wakiwa katika
eneo la shule hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa polisi wa
mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 4
mwaka huu, majira ya saa 5 asubuhi.
Msikhela alifafanua kuwa wanafunzi 71 ndio waliopatwa na
mkasa huo, ambapo walikimbizwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi na matibabu
zaidi.
Alisema kati ya hao watoto ambao hali zao zilikuwa mbaya, watano
wamelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga, na sita wamelazwa hospitali ya
misheni Jimboni iliyopo mjini hapa.
“Baadhi yao ambao waliumwa na nyuki waliruhusiwa kwenda
nyumbani, lakini hawa wengine ilibidi walazwe kwa ajili ya matibabu zaidi
kutokana na hali zao kutokuwa nzuri, lakini taarifa nilizonazo hapa wanaendelea
vizuri huenda nao muda wowote wataruhusiwa”, alisema Msikhela.
Pamoja na mambo mengine, aliwataja wanafunzi waliolazwa katika
hospitali ya wilaya ya Mbinga kuwa ni; Linah Hyera (12), Mussa Mfilinge (6),
Shani Abbasi (5), Faustin Charles (6) na Jibriel Kamtande (6).
Wengine waliolazwa katika hospitali ya misheni Jimboni ni;
Elizabeth Ndunguru (13), George Michael (7), Fabian Ndunguru (6), Happy Mapunda
(5), Katarina Kiwali (13) na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Khadija (10).
Hata hivyo, Msikhela aliongeza kuwa chanzo cha nyuki hao
kuvamia katika eneo la shule ya msingi Mahela, kilitokana na baadhi ya
wanafunzi kwenda kuwachokoza eneo jirani ambalo walikuwa wameweka makazi yao,
katika mti ambao upo jirani na shule hiyo.
No comments:
Post a Comment