Gaudence Kayombo, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma. |
Mbinga.
GAUDENCE Kayombo ambaye ni Mbunge wa jimbo la Mbinga mkoani
Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameendelea kujikuta akiwa
katika wakati mgumu kufuatia baadhi ya wapiga kura wake wa jimbo hilo,
kuendelea kumlalamikia kwamba tokea achaguliwe katika uchaguzi mkuu uliopita
hajawahi kuwatembelea kwenye maeneo yao, jambo ambalo wanakosa imani naye.
Aidha wapiga kura hao walimweleza kuwa, fedha zilizotolewa
na shirika la hifadhi ya jamii (NSSF) kwa ajili ya kuwakwamua wakulima wa
kahawa ambao wamejiunga kwenye vyama ushirika, hawajanufaika nazo kutokana na
kulipwa bei ndogo licha ya fedha hizo kutolewa na shirika hilo kwa riba nafuu.
Walisema wanashangaa kuona malipo waliyolipwa katika msimu
wa mavuno ya kahawa mwaka huu shilingi 4,500 ni kidogo, tofauti na makampuni
binafsi yamekuwa yakilipa kwa bei nzuri kuanzia shilingi 4,700 hadi 5,000 kwa
kilo moja ya kahawa huku yakilipa riba kubwa kwa fedha wanazokopa benki.
Hayo yalijitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana
katika kata ya Nyoni wilayani Mbinga, huku wananchi wa kata hiyo wakizomea pale
Kayombo aliposimama na kuanza kuwaeleza kwamba, yeye alikuwa akimtuma katibu
wake kuja kuwatembelea, kuzungumza na wananchi kwa lengo la kusikiliza kero
mbalimbali na baadaye aweze kuzifanyia kazi.
“Mheshimiwa Mbunge tokea uchaguliwe hatujawahi kukuona
katika kata hii, hivi karibuni mmehamasisha wakulima wa kahawa tujiunge na NSSF
tutoe michango ili tuweze kupata mikopo yenye riba nafuu kwa sisi wakulima wadogo
wadogo ambao tumejiunga katika vyama vya ushirika, lakini tunasikia tu mikopo
imetolewa kwa riba nafuu lakini hatunufaiki nayo”, walisema.
Kwa upande wake Mbunge huyo aliposimama na kujibu juu ya
hoja hizo walizozitoa wananchi wake, alisema yeye amefanya mambo mengi ya
kimaendeleo katika wilaya hiyo huku akimsifia Mkurugenzi mtendaji Hussein Ngaga
na Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga kwamba wanasimamia ipasavyo maendeleo ya
wanambinga, ambapo wananchi hao ghafla waliendelea kuzomea huku wengine
wakisikika na kusema hatukuelewi kwa hayo unayotuambia.
Licha ya Mbunge Kayombo kutumia muda mwingi kujitetea mbele
ya wapiga kura wake katika mkutano huo, bado walikuwa hawamwelewi huku wengine
wakionekana kutoridhika na majibu aliyokuwa akiyatoa mbele yao.
Hivi karibuni hata wafanyabiashara wa wilaya ya Mbinga, pia
walimlalamikia Mbunge huyo katika kikao chao walichoketi mjini hapa, kwamba
tokea achaguliwe pamoja na kumpelekea taarifa wakitaka kuzungumza naye, yeye
amekuwa akiwajibu amebanwa na majukumu ya kikazi yupo safarini, hivyo anakosa
nafasi ya kukaa pamoja na kuzungumza nao.
No comments:
Post a Comment