Jenista Mhagama. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jenista
Mhagama amewataka viongozi wa Jumuiya ya wazazi, vijana na umoja wa wanawake
Tanzania (UWT) kuhakikisha wanafanya kazi ya kuhamasisha wananchi, kwenda
kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kuipigia kura katiba
pendekezwa, ili kutoa fursa ya upigaji kura kwa wananchi wengi hasa
katika kipindi cha uchaguzi mkuu ujao.
Jenista ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho, kupitia
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alitoa wito huo, wakati alipokuwa kwenye
hafla fupi ya kupongezwa kwake kuwa katika nafasi hiyo ya uwaziri, iliyofanyika
kwenye ukumbi wa mikutano wa parokia ya Bombambili, Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wote wa jumuiya za CCM,
ambapo alisema pamoja na mambo yote ya maendeleo ambayo yanafanywa na serikali,
kazi iliyobaki katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ni kuhakikisha
wananchi wanajiandikisha kwenye daftari la kupigia kura, pamoja na kuipigia
kura katiba pendekezwa.
“Kama viongozi wa jumuiya za chama hiki tutasimama kidete
kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha kwenye daftari hili, tutakuwa
tumetoa fursa kubwa kwa wapiga kura kushiriki kikamilifu katika zoezi hili,
ambalo lipo mbele yetu na hatimaye kukifanya chama chetu kiendelee kushika dola”,
alisema Jenista.
Aidha Waziri huyo licha ya kutoa wito huo, aligawa baiskeli
19 zenye thamani ya shilingi milioni 2.2 kwa jumuiya ya wazazi ikiwa ni
mwendelezo wa ahadi zake ndani ya chama, ambapo katika kipindi cha nyuma tayari
alishagawa baiskeli hizo kwa jumuiya nyingine za vijana na UWT kwa kila kata,
kwenye jimbo lake.
Kwa upande wake katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Songea, Rajabu Uhonde
alipozungumza kwenye hafla hiyo alisema kuwa chama chake kimejipanga vizuri
kuhakikisha maagizo yote yaliyotolewa toka ngazi ya taifa yanafanyiwa
kazi, kwa utekelezaji na aliwaonya wale wote ambao wameonesha nia ya
kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao,
wasubiri mpaka muda utakapofika vinginevyo wakionekana wanajipigia debe kabla
ya wakati, watachukuliwa hatua za kinidhamu ndani ya chama.
No comments:
Post a Comment