Na Steven Augustino,
Njombe.
TAARIFA potofu kuhusu yale yanayofanywa katika awamu ya tatu,
katika mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) kwamba umezifanya baadhi ya kaya
maskini hapa nchini, zinazokidhi vigezo vya kuwezeshwa kiuchumi kuwa zimekosa fursa ya
kunufaika na mpango huo, imeelezwa kuwa sio kweli bali ni upotoshaji katika
jamii.
Mkurugenzi mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema
mpango huo ulizinduliwa Agosti 15 mwaka 2012 na Rais Jakaya Kikwete na kuanza
kutekelezwa Februari 2013 ambapo unalenga kuzinusuru kaya masikini, kwa
kuzisaidia fedha ili zipate huduma mbalimbali ikiwemo elimu, afya na maji.
Akifungua kikao cha kazi cha siku mbili mjini Njombe jana,
ambacho kimewashirikisha waratibu wa mpango huo, wahasibu, maafisa ufuatiliaji
na wanahabari, Mwamanga alisema baadhi ya kaya maskini zimekuwa zikidanganywa
kwamba fedha zinazotolewa kupitia mpango huo ni za Freemasons.
Washiriki hao ambao wakakuja na mikakati ya pamoja ya kuelimisha
jamii juu ya malengo na manufaa ya mpango huo, katika kupunguza umaskini nchini
wanatoka katika Halmashauri za mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Iringa na Njombe.
“Kwa wasio na elimu sahihi juu ya mpango huu wanaogopa
kujiunga na mpango kwa sababu ya taarifa hizi potofu, na hivyo familia zao
kukosa uwezeshaji huu ambao tunataraji kuutekeleza sasa,” alisema.
Ili kuondokana na upotoshaji huo, TASAF itahakikisha
inawatumia wanahabari katika maeneo husika ili wasaidie kufikisha kwa umma
taarifa sahihi za mpango huo, ambao ni mmoja kati ya mipango mingi inayolenga
kufikia lengo namba moja la millennia katika kukabiliana na umasikini.
Mpangu huo ni wa miaka kumi, Mkurugenzi huyo alisema kaya
milioni moja zinazoishi katika mazingira duni ya umaskini, zitafikiwa na
kuwezeshwa hapa nchini.
Alisema mpango huo una sehemu kuu tano, ikiwemo ya
uhawilishaji fedha kwa kutoa ruzuku kwa kaya hizo zenye watu wenye uwezo wa
kufanya kazi, kujenga na kuboresha miundombinu inayolenga sekta ya elimu, afya
na maji, na kujenga uwezo katika ngazi zote za utekelezaji.
Alisema utawezesha pia kaya maskini hususan watoto chini ya
miaka mitano na wajawazito kupata lishe bora, huduma za afya, elimu na ajira
kwa kupitia ruzuku za aina mbili, ya msingi na ya kutimiza masharti maalumu.
“Hizo ndio kazi zinazofanywa katika mpango huu, na fedha za
kutekeleza hayo yote zinatolewa na serikali yenyewe kwa kushirikiana na wadau
wake mbalimbali ikiwemo benki ya dunia, hapa hakuna Freemason kama ambavyo baadhi
ya watu wamekuwa wakisema na kupotosha jamii,” alisema Mwamanga.
No comments:
Post a Comment