Thursday, February 26, 2015

SHAMBA LA BHANGI LAMFIKISHA PABAYA AKAMATWA AWEKWA MAHABUSU



Na Amona Mtega,
Songea.

OSWALD Komba (61) maarufu kwa jina la Kibastola, mkazi wa kijiji cha Lipaya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo, kwa tuhuma ya kujihusisha na biashara haramu ya bhangi ambayo alishikwa na miche mingi, ikiwa imepandwa kwenye shamba ambalo inadaiwa kuwa ni la kwake lenye ukubwa wa ekari moja.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 20 mwaka huu majira ya mchana, huko katika kitongoji cha Kilombero kijiji cha Lipaya wilayani humo. 

Msikhela alisema kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema, jeshi la polisi lilikwenda kijijini hapo na kuendesha msako mkali ndipo walipobaini shamba hilo lenye miche mingi ya bhangi, ambalo nila mtuhumiwa huyo.


Alisema kuwa baada ya kuliona shamba hilo, polisi majira ya saa nane mchana waliingia shambani humo na kuing’oa na baadaye kuteketezwa kwa moto.

Mtuhumiwa hivi sasa anashikiliwa katika kituo kikuu cha Polisi Songea mjini, na kwamba wakati wowote kuanzia sasa atafikishwa mahakamani, kwa ajili ya kujibu tuhuma inayomkabili. 

Hata hivyo Kamanda huyo wa polisi mkoani Ruvuma, amewataka wananchi kuendelea kuwa raia wema, kwa kufichua maovu ambayo yanafanywa na watu wasiolitakia mema taifa hili.

No comments: