Na Stephano Mango,
Songea.
MADIWANI katika Halmashauri ya Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma, wamepitisha bajeti ya shilingi 41,886,830,984
kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali vya mapato, ambayo itatumika, kipindi cha
mwaka 2015/2016.
Akisoma bajeti hiyo kwenye kikao cha baraza la madiwani,
kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo mchumi wa Manispaa
hiyo, Raphael Kimary alisema mchanganuo wake, unatokana na vyanzo vya mapato vya
ndani katika halmashauri kiasi cha shilingi 3,259,613,000.
Kadhalika alieleza kuwa mishahara ni shilingi 24,710,969,400
matumizi mengine toka serikali kuu shilingi 2,296,844,000 ambapo ruzuku ya
miradi mbalimbali ya maendeleo shilingi11,619,404,584 ikiwemo na vyanzo vya ndani vya halmashauri
hiyo ni shilingi 3,259,613,000.
Kimary alifafanua kuwa vipaumbele vyao ni kukamilisha
miradi viporo ambayo haikukamilika ujenzi wake, yakiwemo majengo ya zahanati na
vituo vya afya, ukarabati wa ofisi kuu, kata na mitaa, ujenzi wa vivuko vya
madaraja, sekondari, shule za msingi, pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu.
Mchumi huyo alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha
mitandao ya barabara kwa kiwango cha lami, kwenye kata mpya ambazo
zimeongezwa ili ziweze kupitika kwa urahisi hasa kwa kata ambazo
zipo mbali na makao makuu na Manispaa hiyo.
Kadhalika wataendelea kutekeleza mpango wa serikali wa
tekeleza sasa kwa matokeo makubwa katika sekta ya kilimo, elimu, maji pamoja na
mapato.
Awali Meya wa Manispaa hiyo, Charles Mhagama mara tu baada
ya madiwani wote kuridhia kupitisha bajeti hiyo aliwataka kuonesha mfano mzuri,
kuwa mstari wa mbele mwaka huu ambao unaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa
madiwani, wabunge na Rais katika kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu shughuli
mbalimbali za maendeleo, ambazo zitaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa manispaa
hiyo kusonga mbele na madiwani wote kurudi kwenye baraza hilo kwa mara
nyingine.
Mhagama ambaye pia ni diwani wa kata ya Matogoro,
alisema hivi sasa ni vyema kila diwani akajitahidi kumalizia viporo vya miradi ya
maendeleo kwa wananchi wake, ili aweze kujenga imani hasa kwa wapiga kura, ambao wataweza kumchagua tena katika chaguzi zijazo.
No comments:
Post a Comment