Na Julius Konala,
Songea.
BAADHI ya Wakandarasi mkoani Ruvuma, wameilalamikia serikali
kupitia Wakala wa barabara Tanzania (TANROAD) mkoani humo, kutokana na
ucheleweshaji wa malipo yao ya kazi walizofanya, katika mwaka wa fedha wa
2014/2015 hali ambayo sasa, inawafanya waishi katika mazingira magumu.
Wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti mjini hapa,
wakandarasi hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe walisema kuwa hali zao hivi
sasa ni mbaya, kutokana na kudaiwa na taasisi za kibenki ambako walikuwa
wamekopa fedha, kwa ajili ya kuendeshea shughuli za miradi waliyopewa na
TANROAD.
Walidai kuwa baadhi yao mali ambazo waliweka kama dhamana, taasisi
hizo za fedha wameanza kutaifisha na kutokana na kuchelewesha kurejesha mikopo waliyokopa
kwa wakati, hali ambayo inawafanya kuwaingiza kwenye umasikini mkubwa na
kuvunja mahusiano baina yao na hata wamiliki wa maduka, ambako walikopa vifaa
vya ujenzi na kukodi mitambo kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli husika.
Walifafanua kuwa kucheleweshwa kwa malipo hayo ya fedha,
kupitia akaunti ya miradi ya maendeleo imewafanya washindwe kuwalipa vibarua, kulipia
fedha za kukodishia mitambo pamoja na gharama za uendeshaji, hivyo wamedai kwamba
kutokana na mitaji yao kuwa midogo wanashindwa kufanya kazi.
Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wenzake, Ally Mohamed
alisema kutokana na waajiri wao kushindwa kuwalipa mishahara yao, kwa
muda mrefu wamekuwa wakikumbana na matatizo mbalimbali, yakiwemo kushindwa
kumudu gharama za matibabu, kuwapeleka watoto wao shule, kulipia kodi ya nyumba
pamoja na kununua mbolea kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo.
“Hali hii imetufanya tuishi katika mazingira magumu sana,
kwani tunashindwa hata kuwa na fedha kwa ajili ya kununua chakula pamoja na kulipa
kodi ya nyumba, jambo hili linatufanya hata kutokuwepo na maelewano mazuri baina
yetu na wamiliki wa nyumba”, alisema Mohamed.
Hata hivyo alipotafutwa Meneja wa TANROAD mkoani Ruvuma,
Abraham Kisimbo kwa ajili ya kutolea ufafanuzi kuhusiana na malalamiko hayo,
hakuweza kupatikana na hata simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila
kupokelewa.
No comments:
Post a Comment