Friday, December 30, 2016

AFARIKI DUNIA BAADA YA NYOKA WAKE KUPIGWA MAWE NA KUUAWA

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mkazi mmoja ambaye anaishi wa mtaa wa Mateka kata ya Mateka Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Denis Komba (26) amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa Songea mkoa hapa, baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na fimbo nyoka aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa jaketi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Komba kabla ya kufariki dunia alikuwa amekodi pikipi ya Kassian Haulle (24) mkazi wa Mpitimbi yenye namba za usajili MC 724 AKB aina ya Sunlg, ili apelekwe nyumbani kwake anakoishi Mateka.

Zubery Mwombeji.
Aidha walipofika eneo ilipokuwa zamani Benki ya Posta mjini hapa barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alianza kuhisi kwamba kuna kitu kinamtekenya na kumgonga gonga sehemu ya mgongoni na kwamba alipogeuka nyuma ili aweze kujua nini, ndipo alimuona nyoka mkubwa amesimamisha kichwa huku akiwa amebebwa na mteja huyo aliyekodi pikipiki yake.

Kwa upande wake Haulle alisema kuwa, mara baada ya kumuona nyoka huyo alilazimika kuruka kutoka kwenye pikipiki hiyo ambapo baada ya kuanguka nyoka huyo alikimbilia kwenye Kalavati la maji machafu lililopo kando kando ya barabara na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada ndipo kundi la vijana wenzake ambao ni waendesha pikipiki walijitokeza na kuwasili katika eneo la tukio hilo kwa lengo la kumsaidia mwenzao.

Kabla ya vijana hao hawafanya jambo lolote marehemu Komba ambaye alikuwa amembeba nyoka huyo, aliwaomba vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo la tukio wasimpige nyoka wake, kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha.


Kufuatia maneno hayo, Haulle alimtoa nyoka huyo ndani ya Kalavati kwa kushirikiana na vijana wenzake walianza kumpiga hadi kufa na ndipo marehemu Komba alipoona nyoka wake anapigwa, alianza kulegea na kuanguka chini ghafla huku akitokwa povu mdomoni na puani.

Habari zinasema kuwa, baada ya Komba kuanguka na kuwa katika hali mbaya alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu hata hivyo, juhudi za madaktari na wauguzi wa hospitali ya Rufaa Songea za kuokoa maisha yake zilishindikana na hatimaye alifariki dunia.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote na ulihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti, katika hospitali hiyo na nyoka aliyeuawa amechukuliwa na idara ya maliasili kwa uchunguzi  zaidi juu ya tukio hilo ili kuweza kubaini kiini na chanzo cha tukio hilo.

Mwombeji alifafanua kuwa kwa upande wa dereva wa pikipiki yeye anaendelea vizuri na anapatiwa matibabu katika hospitali hiyo ya Rufaa.

Vilevile alisema kuwa ametoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, huku akiwataka waache kumiliki nyara za serikali zinazoweza kuwaletea madhara kama vile majeraha au vifo.

Katika tukio jingine mkazi mmoja  wa kijiji cha Mdunduwalo, Joseph Charles (27)amefariki dunia kwa kuchomwa  na kitu chenye ncha kali tumboni na mtu aliyefahamika kwa jina la Oddo Komba (34) ambaye ni mkazi wa Mhepai Peramiho baada ya kuhitilafiana wakati wakitoka kunywa pombe za kienyeji.

Kamanda huyo wa Polisi alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Disemba 26 mwaka huu majira ya saa moja usiku katika kijiji cha Mtyangimbole kata ya Gumbiro halmashauri ya wilaya ya Madaba wilayani Songea mkoani humo, ambapo chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi uliotokea njiani kati yao wakati wakiwa wanarudi nyumbani kutoka kwenye klabu zinazouza pombe za kienyeji.



No comments: