Saturday, December 24, 2016

WAHASIBU HALMASHAURI ZA WILAYA WATAKIWA KUACHA KUWA MIUNGU WATU

Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

AGIZO limetolewa kwa Watunza fedha wote waliopo katika Halmashauri za wilaya hapa nchini, kutimiza wajibu wao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kazi za serikali na kuacha kuwa miungu watu.

Vilevile wametakiwa kuvunja madaraja na minyororo ya ubinafsi, badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia taratibu husika na maadili ya utumishi wa umma.

Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, katika ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

Waziri huyo alisema kuwa katika halmashauri kumekuwa na tabia kwa baadhi ya Wahasibu kutoa taarifa za uongo kwamba, mfumo wa ulipaji malipo (Epicor) pale malipo husika yanapotakiwa kufanyika umekuwa ukisumbua jambo ambalo sio la kweli hivyo wanapaswa kubadilika.


“Wahasibu mmekuwa na ukiritimba wa namna hii, haya yote yamekuwa yakifanyika kwa lengo la kutengeneza mianya ya rushwa sasa tunataka mbadilike fanyeni kazi kwa kufuata misingi bora iliyowekwa na serikali kabla hamjachukuliwa hatua za kinidhamu”, alisisitiza.

Kadhalika amewataka maofisa manunuzi nao wazingatie sheria na taratibu zilizowekwa katika utendaji wao wa kazi na sio kufanya michakato ya ugawaji wa tenda kwa njia za upendeleo ili waweze kupewa rushwa.

Wakati huo huo, Jaffo aliongeza kuwa katika halmashauri mpya ya mji wa Mbinga serikali imetenga shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi zake hivyo ameutaka uongozi wa halmashauri hiyo kukaa na wadau wake (wananchi) na kufanya majadiliano ambayo yataweka makubaliano mazuri ni wapi ofisi hizo zijengwe.


Alisema kuwa ni kosa kwa watendaji au viongozi kuketi peke yao na kufanya maamuzi ambayo hayana maslahi kwa wananchi juu ya ujenzi wa ofisi hizo ambapo amewataka kuwashirikisha wadau husika ili kuweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima kwamba ni eneo gani linafaa kwa ajili ya ujenzi huo.

No comments: