Sunday, December 18, 2016

MWEKA HAZINA NA WENZAKE SONGEA WASIMAMISHWA KAZI KWA TUHUMA YA KUBADILI MATUMIZI YA FEDHA BILA KUPEWA IDHINI NA KAMATI HUSIKA



Julius Konala,     
Songea.

BARAZA maalum la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, limewasimamisha kazi kwa muda usiojulikana watumishi wake watatu wa halmashauri hiyo kwa ajili ya kupisha uchunguzi, dhidi ya tuhuma zinazowakabili za kubadili matumizi ya fedha bila kupewa idhini na kamati ya fedha, uchumi na mipango.

Watumishi hao wamesimamishwa juzi katika kikao maalum cha baraza hilo kilichoketi kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo mjini hapa, chini ya Mwenyekiti wake Rajab Mtiula na kuhudhuriwa na sekretarieti ya mkoa huo pamoja na wakuu mbalimbali wa idara wa wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Rajab Mtiula aliwataja watumishi waliosimamishwa kazi kuwa ni Wenisalia Swai ambaye ni Ofisa maendeleo ya jamii, Mwajuma Sekelela mweka hazina na Amina Njogela Ofisa ugavi na manunuzi wote wa halmashauri ya wilaya ya Songea.


Mtiula alifafanua kuwa Wenisalia Swai amesimamishwa kazi kutokana na kuidhinisha fedha kinyume na miongozo husika ambazo zilikuwa zimepokelewa kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha afya Mhukuru, wakati alipokaimu nafasi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kwa lengo la kumlipa mkandarasi aliyejenga jengo la makao makuu ya halmashauri hiyo.

Kadhalika Mwajuma Sekelela naye amesimamishwa kutokana na kosa la kushindwa kumshauri Kaimu mkurugenzi wa wakati huo asifanye hivyo, huku Amina Njogela ambaye alikuwa Ofisa ugavi na manunuzi amesimamishwa kwa kosa la kuchelewesha zabuni ya mradi wa umwagiliaji.

Alisema kuwa sababu nyingine iliyopelekea wasimamishwe kazi ni kutumia fedha za utekelezaji wa mradi wa skimu hiyo ya umwagiliaji, kumlipa mkandarasi aliyejenga jengo la makao makuu ya halmashauri ya wilaya hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Songea Simoni Bulenganija alisema kuwa atahakikisha anafuata taratibu, kanuni na sheria za utumishi wa umma katika kuwachukulia hatua za kinidhamu bila ya kumuonea mtumishi yeyote.

Hata hivyo baraza hilo la madiwani limeazimia pia kuunda timu kwa ajili ya uchunguzi zaidi, kwa lengo la kubaini kama kuna ubadhirifu wowote wa fedha za miradi ya wananchi ndani ya halmashauri hiyo ili wahusika wachukuliwe hatua za kinidhamu ikiwa pamoja na kuwafikisha mahakamani.

No comments: