Thursday, December 1, 2016

MADIWANI SONGEA WAPITISHA OMBI LA KUKIPANDISHA HADHI KITUO CHA AFYA MJIMWEMA KUWA HOSPITALI

Ni moja kati ya sehemu ya jengo la kituo cha afya Mjimwema Songea.
Na Gideon Mwakanosya,       
Songea.

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea  mkoani Ruvuma limeridhia na kupitisha ombi la kukipandisha hadhi kituo cha afya Mjimwema na kuwa hospitali ya halmashauri ya Manispaa hiyo.

Ombi hilo liliwasilishwa katika baraza hilo ili hatua nyingine ngazi za juu ziweze kuendelea na kuthibitishwa kuwa hospitali kamili.

Aidha kupandishwa huko na kuwa hospitali ni agizo lililotolewa Januari 11 mwaka huu na Waziri wa afya, ustawi wa jamii, jinsia, watoto na wazee Ummy Mwalimu alipotembelea kituo hicho.

Waziri Mwalimu aliagiza hayo kwa kuutaka uongozi husika wa Manispaa hiyo kuwasilisha katika Wizara yake ombi hilo ili liweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu husika na hatimaye kufikia maamuzi ya mwisho ya kituo cha afya Mjimwema kuwa hospitali ya wilaya katika Manispaa hiyo.


Kwa mujibu wa kikao kilichoketi hivi karibuni kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini hapa kikiongozwa na Meya wa Manispaa hiyo, Abdul Mshaweji kilipokea taarifa hiyo na kuidhinisha upandishaji hadhi wa kituo hicho.

Meya huyo alifafanua kuwa lengo la kuwa hospitali ya wilaya ni kuweza kuboresha huduma mbalimbali za afya ambazo hazipatikani kwenye kituo cha afya na sababu za msingi kuomba kuwa hospitali ni kuiwezesha halmashauri ya Manispaa ya Songea kuwa na hospitali ya wilaya ambayo itaweza kuhudumia wananchi wengi hasa wale wanaotoka katika maeneo ya pembezoni.

Kwa ujumla kituo cha afya Mjimwema kilianzishwa Aprili 8 mwaka 2002 ambapo kinahudumia wakazi zaidi ya 31,091 kati ya hao 1,213 ni watoto chini ya mwaka mmoja na kwamba 5,845 ni watoto chini ya miaka mitano huku 1,275 ni akina mama wajawazito.

Kituo cha afya Mjimwema kina jumla ya majengo nane yakiwemo jengo la wagonjwa wa nje, wodi ya watoto na wanawake, wodi ya wazazi na huduma za kujifungua, jengo la kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto na wodi ya wanaume, jengo la utawala, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba mbili za watumishi na jengo la upasuaji.


Mshaweji alieleza kuwa kituo hicho cha afya kina jumla ya watumishi 110 wa kada mbalimbali na kwamba kinatoa huduma mbalimbali za afya lakini hivi sasa huduma ambazo hazitolewi katika kituo hicho cha afya ni pamoja na huduma ya upasuaji licha ya kwamba jengo husika limekamilika lakini vifaa bado havitoshelezi kwa ajili ya mahitaji husika.

No comments: