Wednesday, December 21, 2016

MANISPAA SONGEA YABAINI KAYA HEWA 2,692 AMBAZO HAZIKUWA NA SIFA YA KUENDELEA KUPEWA RUZUKU YA TASAF

Baadhi ya Wanufaika wa ruzuku ya kaya maskini wakiwa katika ofisi za serikali ya kijiji mtaa wa Oysterbay kata ya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wakisubiri kupewa ruzuku na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). 
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao unahudumia kaya maskini katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, umeengua kaya hewa 2,692 ambazo zimebainika kwamba hazikuwa na sifa ya kuendelea kupewa ruzuku ya kuhudumia kaya maskini.

Kaya zilizoenguliwa ni kati ya 7,695 zilizokuwa zinanufaika na ruzuku hiyo ambapo hivi sasa baada ya uhakiki kufanyika, kaya zenye sifa ya kupata fedha kutoka kwenye mfuko huo zimebakia 5,003.

Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alibainisha hayo jana alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu na kueleza kuwa tayari shilingi milioni 277 zimetolewa kwa kaya maskini 5,003 zilizopo katika mitaa 53 ya Manispaa ya Songea ambayo ipo kwenye mpango wa kupewa ruzuku.


Vilevile alisema kuwa kaya ambazo zimeondolewa kwenye mpango huo zimekabidhiwa barua rasmi juu ya kuenguliwa kwao, baada ya uhakiki wa nyumba kwa nyumba kufanyika ambao ulibaini kaya hizo kutokuwa na sifa.

Midelo aliongeza kuwa kati ya kaya zilizoenguliwa ilibainika kuwa kaya 1,599 hazikuwa maskini, kaya 342 walihama katika maeneo yao ya awali waliyokuwa wakiishi, kaya 110 walifariki dunia, kaya 417 zilibainika kuwa ni hewa na kaya 144 hazikuwepo kwenye uhakiki huo.

Pamoja na mambo mengine halmashauri ya Manispaa ya Songea imeendelea kupokea fedha kwa ajili ya mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia mradi wa TASAF awamu ya tatu, ikiwa ni lengo la kupunguza umaskini kwa watu wasiojiweza na kwamba hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu zaidi ya shilingi bilioni 1.6 zilipokelewa katika Manispaa hiyo.




No comments: