Sunday, December 18, 2016

WASHAURIWA KUTUMIA NISHATI YA MAKAA YA MAWE

Na Kassian Nyandindi,            
Mbinga.

JAMII hapa nchini imeshauriwa kuacha kukata miti hovyo na kuitumia kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, badala yake wanapaswa kutumia nishati ya makaa ya mawe kwa ajili ya shughuli zao za kila siku, hatua ambayo itasaidia kutunza mazingira na kuepukana na athari kubwa ya uharibifu wa mazingira kunakosababishwa na matumizi ya kuni.

Kufuatia hali hiyo serikali kupitia wataalamu wake imeombwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi, juu ya madhara ya ukataji miti na matumizi ya kuni kwa ajili ya kupikia au shughuli nyingine za kibinadamu.
Makaa ya mawe.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Leah Kayombo ambaye ni Meneja wa shirika lisilokuwa la kiserikali, Mbalawala Women Group Organisation lililopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  waliotembelea kuona namna shirika hilo, lilivyofanikiwa katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi na uchimbaji wa makaa ya mawe kijijini humo.


Kayombo alisema kuwa kutokana na kasi  kubwa ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu katika  vijiji vinavyozunguka mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka, kuanzia mwaka 2014 hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu wameweza kupanda miti 36,000 pamoja na kuanzisha vitalu vya miti ambayo imesambazwa bure katika taasisi za umma kama vile shule, hospitali na watu binafsi ili nao waweze kuipanda katika maeneo yao.

Alisema kuwa lengo la kuanzisha mradi wa upandaji  na uanzishwaji wa vitalu vya miti ni kuisaidia serikali katika kupambana na uharibifu wa mazingira, ili watu waweze kuipanda na kuweza kuhifadhi uoto wake wa asili katika misitu hata kwenye vyanzo vya maji.

Kayombo aliafanua kuwa shirika hilo linaundwa na serikali ya vijiji vya Ruanda na Ntunduaro kwa kushirikiana na Mwekezaji wa mgodi wa Tancoal Energy na kwamba, wamekuwa wakijishughulisha na utengenezaji wa makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi ya majumbani na kuweza kuajiri baadhi ya vijana ambao wengine wana ajira za muda na kudumu.

Licha ya kupata mafanikio hayo alieleza kuwa bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile  wateja wa uhakika, ukosefu wa gari  lenye uwezo wa kubeba kiasi kikubwa cha makaa ya mawe kwenda kwa wateja pamoja na  kukosekana kwa huduma ya maji, jambo  ambalo linawafanya kutegemea msaada kutoka kwa mwekezaji wa mgodi huo ambaye huwasaidia pale wanapokwama jambo fulani.

Kwa mujibu wa Kayombo ni kwamba, wameshaanza kuchukua hatua ya kukabiliana na tatizo hilo kwa kuanza kuchimba visima virefu vitakavyosaidia kuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.

Hivi sasa kuna baadhi ya watu kutoka katika baadhi ya mikoa hapa nchini, wameonesha nia ya kuhitaji makaa hayo wanayotengeneza kwa ajili ya shughuli za kupikia ambapo ni kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Songea pamoja na wateja kutoka ndani ya wilaya ya Mbinga.

Kwa upande wake Meneja uzalishaji wa kikundi hicho, Hajiri Kapinga ameishukuru Kampuni ya Tancoal Energy, kwa kuwapatia msaada wa mashine ya kutengeneza makaa hayo, kujenga maabara ya kufanyia shughuli hizo za utengenezaji mkaa na mtaalamu aliyebobea katika utengenezaji wa makaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.


No comments: