Wednesday, December 7, 2016

SERIKALI YATUMIA MILIONI 55 KUENDELEZA MIRADI YA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA SONGEA

Na Mwandishi wetu,        
Songea.

KATIKA kuendeleza miradi ya maji safi na usafi wa mazingira, serikali hapa nchini imetoa zaidi ya shilingi milioni 55 kwa halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kwa ajili ya kuendeleza miradi hiyo kwa manufaa ya wananchi wake.

Aidha imefafanuliwa kuwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji na usafi wa mazingira kwa lengo la kuzijengea uwezo Jumuiya za Watumiaji Maji (COWSO) na usimamizi wa maji.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa fedha hizo tayari zimetumika katika suala la uchangiaji huduma ya matumizi ya maji katika mitaa ya Mahilo, Muhombezi, Ruhuwiko Kanisani na Chandarua.


Alisema shilingi milioni 5.2 zimepelekwa kwa ajili ya ujenzi wa choo katika zahanati ya Bombambili na shilingi milioni 9.9 zimepelekwa shule ya msingi Mateka, Msamala na Kawawa kwa ajili ya ukarabati wa vyoo vya shule hizo zilizopo mjini hapa.

Mkoa wa Ruvuma unakadiriwa kuwa na wakazi 1,497,853 kati ya hao wakazi 851,034 sawa na asilimia 57 tu, ndiyo wanaopata maji safi na salama kwa mujibu wa takwimu za kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.

Midelo aliongeza kuwa katika maeneo ya vijijni wakazi wanaopata huduma ya maji safi na salama ni asilimia 54.4 huku kwa wale wanaoishi mjini hupata kwa asilimia 68.1.

Hata hivyo hivi karibuni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge aliwaagiza Wakurugenzi wote waliopo katika halmashauri za mkoa huo, kusimamia kikamilifu miradi yote ya maji ambayo imekamilika ujenzi wake na ile ambayo inaendelea kujengwa, ili kuweza kuwatendea haki wananchi ambao wanasumbuka kutafuta maji umbali mrefu.


No comments: