Tuesday, December 27, 2016

WAFANIKIWA KUSAMBAZA VYANDARUA KWA WATOTO MASHULENI

Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

KATIKA kuhakikisha kwamba ugonjwa hatari wa malaria unaendelea kudhibitiwa, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu, imesambaza vyandarua 42,174 kwa watoto wa shule za msingi na sekondari zilizopo wilayani humo. 

Aidha hali ya maambukizi ya ugonjwa huo katika wilaya hiyo imepungua kwa asilimia 24 kutokana na wataalamu wa afya kuendelea kuhimiza wananchi kuweka mazingira yao wanayoishi katika hali ya usafi wakati wote ili kuepukana na mazalia ya mbu wanaobeba vimelea vya ugonjwa huo.

Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Mbinga, Sarah Komba alisema hayo wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya halmashauri yake ilivyojiwekea mikakati ya kupambana na ugonjwa huo kwa lengo la kupunguza maambukizi na vifo visivyokuwa vya lazima vitokanavyo na malaria.


Komba alisema kuwa katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka jana wagonjwa wa nje 53,671 waliweza kupatiwa matibabu ambao walionekana kuwa na vimelea vya ugonjwa huo.

“Katika kufanikisha hili tumekuwa tukihamasisha kufanya usafi wa mazingira ili kuweza kupunguza mazalia ya mbu na kutoa elimu ya afya kupitia mikutano mbalimbali katika vituo vya kutolea huduma”, alisema.


Hata hivyo changamoto kubwa wanayokabiliana nayo hivi sasa ni upungufu wa watumishi 253 ambapo waliopo ni 184 huku mahitaji halisi yakiwa ni 437 ambapo wanaiomba serikali, iendelee kukabiliana na hali hiyo kwa kuajiri watumishi wengine ili kuweza kufikia malengo husika katika sekta hiyo ya afya.

No comments: