Tuesday, December 20, 2016

MWANAFUNZI CHUO KIKUU SONGEA AKUTWA AKIWA AMEFARIKI DUNIA BAADA YA KUJINYONGA MSITUNI

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Yakobo (AJUCO) tawi la Songea mkoani Ruvuma, Henry Mwelang’ombe (24) ambaye ni wa mwaka kwanza amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba aina ya manila, kwenye msitu uliopo nyuma ya shule ya sekondari ya wasichana Songea iliyopo mjini hapa.

Habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa na mwalimu mmoja anayefundisha katika sekondari hiyo ya wasichana ambaye hakutaka kumtaja jina lake.

Mwombeji alisema kuwa mwalimu huyo alikuwa akielekea shambani kwake majira ya asubuhi ambapo ghafla aliukuta mwili wa marahemu huyo ukiwa unaning’inia kwenye mti katika msitu huo Disemba 18 mwaka huu majira hayo ya asubuhi.

Kamanda huyo wa Polisi hapa mkoani Ruvuma alifafanua kuwa mwalimu huyo baada ya kuona tukio hilo ambalo lilimshitua, alichukua jukumu la kutoa taarifa kwa majirani wanaozunguka eneo hilo ambapo baadaye walilazimika kwenda kutoa taarifa kituo kikuu cha Polisi Songea mjini na askari walikwenda huko, kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari ambaye alithibitisha kuwa Henry amefariki dunia kutokana na kujinyonga huko.


Alifafanua kuwa mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa ukiwa umeharibika vibaya, ambapo inadaiwa kuwa marehemu alikuwa amejinyonga siku kadhaa zilizopita ambapo waliukuta pia ujumbe uliokuwa umeandikwa kwenye daftari dogo ambalo lilikuwa na maneno yafutayo;

“Nini maana ya utu, acha nife siwezi kuvumilia, walionitenda nawaona acha nife tu mimi. Utu sio mavazi marafiki wengi ni wanafiki tulikuwa safari moja sasa tumetengana, yote sababu ya pesa, fikiria ungekuwa wewe, nilihisi narekodiwa toka Mbeya sasa ni kweli tuache siasa tubaki kwenye ukweli,

“Nafanya haya sababu sikutaka viungo vyangu vionekane hadharani, hii ni kwa sababu ya kulinda utu na heshima, ulemavu umekuwa tatizo kwangu, sikupenda nijione, sitaki nijione mimi ni mkosaji nisamehe Allah”, ulisema ujumbe huo.

Aidha katika chumba alichokuwa akiishi kulipatikana pia ujumbe mwingine wa maneno yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili yaliyosomeka hivi; “My Dream B me true na inauma sana”.

Kadhalika jitihada za mwandishi wa habari hizi kumpata Mkuu wa chuo cha AJUCO tawi la Songea, Dkt. Longino Lutagwelela ziligonga mwamba baada ya kuelezwa kwamba yupo Mwanza kikazi lakini mlezi wa chuo hicho Michael Sinienga alipohojiwa alisema kuwa taarifa za tukio hilo amezipata Disemba 18 mwaka huu majira ya saa tano asubuhi, wakati alipokuwa akitokea kanisani baada ya kuambiwa na wafanyakazi wenzake.

Sinienga alisema kuwa Henry alikuwa ni mwanachuo wa chuo hicho mwaka wa kwanza ambapo alikuwa anasomea shahada ya Sanaa na Ualimu na kwamba taarifa za tukio hilo, tayari ameshaujulisha uongozi wa chuo na taratibu husika zinatekelezwa za kuusafirisha mwili wake kuelekea Chimala wilayani Mbarali mkoani Mbeya, nyumbani kwa wazazi wake ambako mazishi yake yanatarajiwa kufanyika.

Kadhalika alipohojiwa kwamba mwanafunzi huyo inadaiwa kuwa alikuwa na tatizo la kutopata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo (HESLB), alifafanua kuwa Marehemu alikuwa miongoni mwa wanafunzi walionufaika na mkopo kutoka katika  bodi hiyo.

Baadhi ya majirani akiwemo mwenye nyumba eneo la Majengo jirani na eneo la chuo hicho ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao ambako marehemu katika uhai wake alikuwa amepanga na kuishi huko walieleza kuwa, ni zaidi ya wiki moja alikuwa hajaonekana pale nyumbani alipokuwa anaishi na kwamba walikuwa wakihisi kwamba alikuwa chuoni akijisomea pamoja na wanachuo wenzake kwa kuwa halikuwa jambo geni kwao kutorudi nyumbani kwa sababu ya kujisomea na wanachuo wenzake.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji alieleza kuwa kupitia idara yake ya upelelezi makosa ya jinai uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika kuhusiana na tukio hilo ili kuweza kubaini chanzo chake na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.


No comments: