Saturday, December 24, 2016

JAFFO: DOKTA MAGUFULI AMEVUNJA REKODI ULIPAJI MADENI NDANI YA NCHI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa tokea nchi hii ipate Uhuru, Rais wa awanu ya tano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amekuwa wa kwanza kuvunja rekodi katika ulipaji wa madeni mbalimbali ndani ya nchi, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 970 ameweza kulipa kwa wakandarasi  na wadeni wengine ambao walikuwa wakiidai serikali.

Suleiman Jaffo ambaye ni Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) alisema hayo jana alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma huku akiongeza kuwa, nchi hii ilifikia mahali pabaya kwa sababu ya madeni hayo na watu wachache kuwa wabinafsi wakitaka kujilimbikizia mali nyingi.

Alifafanua kuwa ufanisi huo wa ulipaji wa madeni umetokana na serikali kuwa imara katika ukusanyaji wa mapato yake, ambapo imekuwa ikikusanya shilingi bilioni 800 kila mwezi.

Hivyo aliwataka watendaji wa serikali ambao walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea muda wao umepita na wanapaswa kubadilika ili waweze kuendana na kasi ya awamu ya tano, ambayo ina malengo ya kusimamia na kutekeleza ipasavyo maendeleo ya wananchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.


“Watumishi wengi walizoea stahili ya uongozi uliopita hivi sasa tunapaswa kubadilika kwenda na wakati kwa sababu Watanzania wanataka mabadiliko, ndio maana wakati mwingine mnaona maamuzi magumu yamekuwa yakifanyika kwa lengo la kuwafikishia maendeleo wananchi wetu”, alisema.

Pia amewataka Wakurugenzi watendaji katika halmashauri za wilaya hapa nchini, kuketi na wakuu wao wa idara na kupanga malengo yenye kuleta tija kwa maendeleo ya wananchi na kwamba, kwa mkuu wa idara ambaye ataonekana kutotekeleza majukumu yake ya kazi ipasavyo achukuliwe hatua ikiwemo kuondolewa katika cheo chake.

Aliongeza kuwa ikiwa wamepewa dhamana na serikali za mitaa watumishi wanapaswa kuzungumza lugha moja na sio viongozi kugawanyika, jambo ambalo linaweza kuwafanya wagombane na kuendeleza mifarakano isiyokuwa ya lazima ambayo inarudisha nyumba maendeleo ya wananchi.

Vilevile akizungumzia juu ya madai mbalimbali ya watumishi alisema kuwa serikali imechukua hatua kwa kuandaa kikosi kazi, ambacho kinafanya uhakiki wa madeni hayo ikiwemo kuondoa wimbi la watumishi hewa.


Hata hivyo alieleza kuwa kila mwezi shilingi bilioni 25 zilikuwa zinaenda kwa watu hewa na kwamba zoezi hilo la uhakiki litakapokamilika watumishi wote wanaoidai serikali watalipwa stahiki zao.

No comments: