Sunday, December 25, 2016

WANANCHI SONGEA WATAKIWA KUPUNGUZA TATIZO LA UTAPIA MLO KWA WATOTO WADOGO

Baadhi ya Wakazi mji mdogo wa Peramiho mkoani Ruvuma, wakisikiliza kwa makini uzinduzi wa kampeni ya kupunguza na kuzuia udumavu kwa watoto.
Na Mwandishi wetu,    
Songea.

WANANCHI wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wametakiwa kuwa na mikakati na mipango thabiti, yenye kulenga kupunguza tatizo la utapia mlo wilayani humo ambao umekuwa ukiwaathiri watoto wadogo katika makuzi yao, kwa kuwafanya waonekane kuwa wamedumaa.

Mwito huo umetolewa juzi na Katibu tawala wa wilaya hiyo, Pendo Daniel alipokuwa akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Peramiho wilayani hapa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupunguza na kuzuia udumavu kwa watoto hao.

Alisema kuwa serikali tayari imekwisha agiza, kutenga na kuongeza bajeti ya lishe katika ngazi zote ikiwemo shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano kwa mwaka na kwamba, maagizo hayo tayari yametolewa kwenye ngazi husika katika halmashauri zote za mkoa huo.


Pendo alifafanua kwamba serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa mstari wa mbele kukabiliana na tatizo la lishe duni hapa nchini, ambapo uchukuaji wa hatua hiyo unajumuisha utoaji wa dawa za vidonge vya kuongeza damu, madini ya chuma na vitamin folic acid kwa wanawake wajawazito.

Alisema kuwa utoaji wa vitamin A pamoja na dawa za kutibu minyoo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na uwekaji wa madini joto katika chumvi, nguvu kubwa imekuwa ikitumika katika uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa umma ambapo wilaya ya Songea, shirika lisilokuwa la serikali Counsenuth hujishughulisha na utoaji huo wa lishe kwa wilaya hiyo na ile ya Madaba iliyopo mkoani hapa.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa lishe mkoani Ruvuma  wa shirika hilo, Fatuma Hamis alisema kuwa tayari kwa kushirikiana na serikali wanaendelea kuhamasisha wananchi, kuwapa elimu ya lishe bora kwa watoto wadogo na hatimaye wameweza kufanikiwa kutokomeza udumavu huo.

Fatuma alieleza kuwa takwimu za utafiti wa masuala ya lishe uliofanywa na shirika lake mwaka 2013 katika wilaya ya Songea zinaonesha kuwa asilimia 37.3 ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili ni wadumavu, ambao wanashindwa kukua na kufikia urefu unaotakiwa kulingana na umri wao.

Mratibu huyo alisema kuwa vilevile takwimu za utafiti masuala ya afya na idadi ya watu mwaka 2015 zinonesha kuwa asilimia 44 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano mkoani hapa, wamedumaa na asilimia 51.8 ya watoto hao wanaupungufu wa damu jambo ambalo linahitaji jitihada kubwa za uhamasishaji ili kuweza kuondokana na tatizo hilo.


No comments: