Sunday, December 18, 2016

MAMA ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUMUUA MWANAYE



Na Gideon Mwakanosya,         
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia, Eva Kapinga (20) ambaye ni mkazi wa wa kata ya Mateka Manispaa ya Songea mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mtoto wake Catherine Kapinga mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, kisha mwanamke huyo kuamua kujichoma na kisu tumboni kwa lengo la kutaka kujiua. 

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Disemba Mosi mwaka huu majira ya jioni katika eneo la mtaa wa Mateka C ambapo Eva baada ya kujichoma kisi hicho amejisababishia jeraha kubwa ambalo limepelekea kulazwa hospitalini.

Mwombeji alifafanua kuwa siku ya tukio hilo Catherine aliuwawa na mama huyo ambaye pia ni mjamzito, na kwamba chanzo cha mauaji hayo bado hakijulikani licha ya kwamba taarifa za awali zinaeleza kuwa Eva alikuwa na malumbano kati yake na mama yake mzazi Sofia Mayunga ambaye alikuwa akimuuliza kwa nini ameamua kushika mimba wakati anajua kuwa ana mtoto mdogo wa umri wa mwaka mmoja, jambo ambalo limfanya kupandwa hasira na kuamua kufanya kitendo hicho.


Kamanda huyo wa Polisi alifafanua kuwa mama huyo baada ya kujichoma kisu tumboni majirani walimpeleka hospitali ya mkoa Songea na taarifa za tukio hilo zilikuwa tayari zimeshafikishwa Polisi na kwamba askari walipofika kwenye eneo la tukio, walimkuta motto Catherine akiwa amekwisha fariki dunia baada ya kuuawa na mama yake.

Vilevile baadaye walipokwenda hospitali hiyo ya mkoa ambako walimkuta Eva akiwa katika hali mbaya ambako madaktari walikuwa wakimpatia matibabu huku akiwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi.

Hata hivyo Kamanda Mwombeji alieleza kuwa Polisi mkoani Ruvuma, inaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo na kwamba utakapokamilika mtuhumiwa Eva atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

No comments: