Wednesday, December 21, 2016

RADI YAKATISHA MAISHA YA MTOTO CREDO WAWILI WANUSURIKA

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MTOTO Credo Adrian Ndomba (4) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Miembeni katika kitongoji cha Majembe kata ya Kitanda Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, amefariki dunia papo hapo baada ya kupigwa na radi na kumuunguza mwili wake akiwa amelala.

Zubery Mwombeji.
Aidha katika tukio hilo ambalo lilitokea nyakati za usiku mtoto mwenzake, Esther Ndomba pamoja na mama yao mzazi, Yustina Ndunguru (30) nao walinusurika kupoteza maisha baada ya radi hiyo iliyoambatana na mvua kuunguza nyumba waliyokuwa wamelala.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alimweleza mwandishi wetu kuwa tukio hilo lilitokea Disemba 18 mwaka huu majira ya usiku ambapo Esther na Yustina, walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali ya halmashauri ya mji wa Mbinga iliyopo mjini hapa kwa ajili ya matibabu zaidi.  


Mwombeji alieleza kuwa baada ya tatizo hilo kutokea Polisi kwa kushirikiana na mganga wa hospitali hiyo ambaye hakumtaja jina lake, walikwenda katika eneo la tukio hilo na kuthibitisha kifo cha mtoto huyo.

Vilevile alifafanua kuwa majeruhi hao wanapatiwa matibabu katika hospitali hiyo na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Kitanda, Zeno Mbunda alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi alisema kuwa baada ya Polisi kuripoti katika eneo la tukio hilo na kuthibitisha mtoto Credo kuwa amefariki, yeye kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo walichukua jukumu la kufanya mazishi.


“Baada ya radi kupiga na kuunguza nyumba yote na kusababisha mauaji kwa mtoto huyu, wengine wamejeruhiwa vibaya na kupelekwa katika hospitali ya mji wa Mbinga kwa ajili ya kupatiwa matibabu”, alisema Mbunda. 

No comments: