Friday, December 30, 2016

WANACHAMA MAHANJE SACCOS WALALAMIKIA WAKAGUZI WA COASCO SONGEA

Na Julius Konala,       
Songea.

WANACHAMA wa chama cha akiba na mikopo Mahanje SACCOS katika Halmashauri ya Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wameilalamikia Ofisi ya ukaguzi wa vyama hivyo COASCO mkoani hapa kwa madai kuwa wameshindwa kutoa taarifa ya ukaguzi wa chama hicho tangu mwaka 2014.

Malalamiko hayo yalitolewa jana na wanachama hao kwenye mkutano mkuu wa 19 wa chama hicho, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Tumaini uliopo mjini hapa, ambapo walidai kuwa hali hiyo inasababisha chama chao kushindwa kupata mikopo na kufanya shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo.

Akichangia hoja katika mkutano huo mshauri wa chama hicho, Nathan Malangalila alisema kuwa vyama vingi vya ushirika wa akiba na mikopo vimekufa kwa sababu ya kukosa usimamizi wenye uongozi makini pamoja na kushindwa kutoa ripoti mbalimbali za ukaguzi.


Malangalila alisema kuwa pamoja na chama chao kutoa fedha kwa ajili ya kufanyia ukaguzi husika, lakini hakuna utekelezaji uliofanyika ambapo maofisa wa COASCO mkoani humo wameonekana wakipokea fedha hizo bila ya kufanya kazi na kupelekea usumbufu kwa wanachama wa Mahanje SACCOS.

“Viongozi wa COASCO wamekuwa wasumbufu kwa kuwa kila wanapoulizwa kuhusiana na taarifa hiyo mara wanasema ipo Dodoma mara ipo Madaba, wakati sio kweli hivi tunaiomba halmashauri ya Madaba kwa kushirikiana na Ofisa ushirika wa halmashauri hii kufuatilia jambo hili na tuweze kupata majibu sahihi”, alisisitiza Malangalila.

Naye Meneja wa Mahanje SACCOS, Kassim Masengo akizungumza katika mkutano huo alisema kuwa inashangaza kuona chama kinatoa gharama kwa ajili ya ukaguzi lakini maofisa waliopewa dhamana wamekuwa wazembe katika kukitembelea chama hicho kwa ajili ya kutoa ripoti za kaguzi zinazofanyika.


Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa chama hicho walisema kuwa kuna kila sababu ya kuwakataa wakaguzi wa COASCO kwa ajili ya kuifanyia ukaguzi ushirika wao kuytokana na kuonesha dhahiri kwamba wameshindwa kufanya kazi hiyo na badala yake watafutwe watu wengine watakaoweza kufanya ukaguzi katika chama hicho.

No comments: