Sunday, September 21, 2014

CHUO KIKUU CHA SAYANSI SONGEA CHA PONGEZWA KWA JITIHADA ZAKE


Na Mwandishi wetu,

Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amekipongeza chuo kikuu cha sayansi ya kompyuta cha Mtakatifu Joseph tawi la Songea mkoani humo, kwa jitihada zake za kuendelea kupanua wigo wa kutoa huduma na kukuza elimu ya juu hapa nchini.

Mwambungu alitoa pongezi hizo alipokuwa akihutubia kwenye mahafali ya tano ya chuo hicho mjini hapa, kwa wahitimu 119 wa shahada na stashahada ambapo alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho, kumesaidia kulipunguzia taifa tatizo la ukosefu wa wataalam wa sayansi hususan katika ukanda wa kusini na taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo kikuu cha sayansi ya kilimo na teknolojia katika sekta ya kilimo, ni jambo jema kwa ustawi wa nchi na uti wa mgongo na mwajiri mkubwa kwa wananchi huku akiwataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Alieleza kuwa katika maisha ya sasa hakuna njia fupi ya kufikia mafanikio katika maisha  zaidi ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa, na kwamba changamoto zilizopo katika chuo hicho zigeuzwe kuwa fursa pekee ya kujipanua na kutoa elimu bora,  huku akiwataka kuboresha mawasiliano ili kukuza wigo wa utatuzi wa changamoto hizo.

Friday, September 19, 2014

MKUU WA MKOA RUVUMA AKUTANA NA MADEREVA PIKIPIKI, ASISITIZA AMANI NA UTULIVU


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, akizungumza na waendesha pikipiki (Maarufu kama  Boda Boda) leo katika ukumbi wa Songea Club uliopo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma. Mwambungu amewataka madereva Boda boda kuepusha ajali za barabarani kwa kufuata sheria, na kutotumiwa na vyama vya kisiasa.

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

BAADA ya siku chache kupita kufuatia tukio la nani amefanya kitendo kiovu cha kurusha bomu la kienyeji katika mtaa wa Msufini Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, na kujeruhi baadhi ya askari Polisi mjini hapa, Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu amekutana na waendesha pikipiki wa manispaa hiyo na kuwataka  kujenga ushirikiano ili kuweza kulinda amani ya nchi dhidi ya maadui ambao hawalitakii mema taifa hili.

Mwambungu amekutana leo na madereva hao maarufu kwa jina la “Boda boda” katika ukumbi wa Songea Club uliopo mjini Songea, akisisitiza kujenga ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kuweza kupata ukweli wa tukio hilo na kuwafanya wakazi wa mji huo, watu wengine (wageni) wanaoingia na kutoka kuondoa hofu na kuishi katika hali ya usalama.

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa jamii ihakikishe kwamba amani utulivu vinatawala miongoni mwao, na pale wanapoona kuna sintofahamu ni vyema watoe taarifa katika vyombo husika vya usalama ili kuweza kubaini uhalifu unaofanyika na hatua ziweze kuchukuliwa haraka dhidi ya wahalifu.

JESHI LA POLISI NCHINI LANYOSHEWA KIDOLE LATAKIWA KUACHA KUNYANYASA WAANDISHI WA HABARI

Rais Jakaya Kikwete wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

















Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

JESHI la Polisi nchini limetakiwa kuacha vitendo vya  kuwanyanyasa waandishi wa habari na kuwafanya wasitekeleze wajibu wao ipasavyo, kufanya hivyo ni kutowatendea haki na kudhalilisha taaluma ya habari.

Sambamba na hilo Jeshi hilo limenyoshewa kidole kwamba limekuwa na historia ya kupiga na kuwafukuza waandishi wa habari, hasa pale wanapotafuta ukweli juu ya matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakitokea miongoni mwa jamii.

Rai hiyo imetolewa na baadhi ya Wananchi wa mkoa wa Ruvuma, walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti kufuatia tukio lililotokea jana makao makuu ya jeshi hilo baada ya waandishi kupigwa, kukimbizwa na mbwa ili wasichukue taarifa za kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe.

Thursday, September 18, 2014

JESHI LA POLISI NCHINI LATHIBITISHA BOMU WALILORUSHIWA ASKARI WAKE MJINI SONGEA LIMETENGENEZWA KIENYEJI

 Eneo la tukio mtaa wa Msufini mjini Songea mkoani Ruvuma, ambako bomu ambalo limetengenezwa kienyeji lilirushwa kwa mkono na watu wasiojulikana Jeshi la Polisi likiwa limezungushia alama.
Askari Ramadhani Ally, akiwa amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea, akielezea kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi mkasa huo ulivyowakuta na askari wenzake wakati walipokuwa doria mtaa wa Msufini mjini hapa,  baada ya kurushiwa bomu ambalo limetengenezwa kienyeji na watu wasiojulikana mpaka sasa.

Na Kassian Nyandindi,
Songea.


JESHI la polisi nchini limethibitisha kuwa kitu kilichokuwa kinadaiwa kuwa ni bomu lililorushwa mjini Songea mkoani Ruvuma, na kuwajeruhi askari wa jeshi hilo mjini hapa kuwa ni la kutupwa kwa mkono.

Tukio hilo lilitokea  Septemba 16 mwaka huu majira ya saa 1.25 usiku katika eneo la Misufini na kuwajeruhi askari polisi watatu kati ya wanne waliokuwa doria na kwamba bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

Akitoa taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo kwa waandishi wa habari mjini hapa, Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai kamishina wa polisi Isaya Mngulu amesema bomu hilo lilirushwa na watu wasiojulikana na kuwajeruhi askari polisi watatu waliokuwa doria siku hiyo.

Mngulu alisema askari hao ni wa kituo kikuu cha polisi mjini Songea ambao aliwataja kuwa ni G.5515 PC John, G7351 PC Ramadhan na WP 10399 Felista ambapo baaada ya kujeruhiwa kwa bomu hilo, walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya matibabu.

KATIBU TAWALA MSAIDIZI MKOANI RUVUMA NA WENZAKE WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA WIZI WA SHILINGI MILIONI 800

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MWENYEKITI wa chama kikuu cha ushirika (SONAMCU) wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma, amefikishwa katika Mahakama ya mkoa huo akiwemo na Katibu tawala msaidizi wa mkoa huo ambaye pia ni afisa ushirika wa mkoa huo, kwa tuhuma za kula njama, kugushi nyaraka na kuiba fedha shilingi milioni 889.

Imedaiwa mahakamani hapo na mwanasheria wa serikali Hamimu Mkoleye mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya mkoa huo Joackimu Tiganga washtakiwa hao wote wawili wanalinganishwa na washitakiwa wengine 14 ambao walikwisha somewa mashitaka na kufanya idadi yao kuwa 16 ambapo wanadaiwa kuiba fedha hizo.

Mkoleye amewataja waliofikishwa mahakamani hapo kuwa ni Ally Athumani Bango (45) Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Namtumbo (SONAMCO) ambacho kinajishughulisha na ununuzi wa zao la tumbaku.

AHUKUMIWA KWENDA JELA BAADA YA KULAWITI



Na Mwandishi wetu,
Songea.

MKAZI mmoja wa Mjimwema Songea mjini mkoani Ruvuma, amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu mkazi wa mkoa huo adhabu ya kifungo cha maisha  kwenda gerezani kwa kosa la kumlawiti msichana mwenye umri wa miaka tisa.

Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa huo, Joakimu Tiganga alisema kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuwa John Mapunda (38) mkazi wa Mjimwema songea mjini bila halali alimlawiti msichana huyo.

DEREVA PIKIPIKI AKUTWA AMEFARIKI DUNIA BAADA KUCHOMWA KISU TUMBONI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MTU mmoja ambaye ni dereva wa pikipiki amekutwa amefariki dunia baada kuchomwa kisu tumboni na kupigwa na kitu kizito kichwani kisha mwili wake kufungwa kamba mikononi na miguuni hatimaye kuunganishwa kwenye mti na watu wasiojulikana.

Tukio hilo lilitokea Septemba 16 mwaka huu majira ya mchana ambapo mwili wa marehemu huyo umetambuliwa kwa jina la Maulid Kuburi (21) mkazi wa kijiji cha Mpandangindo Songea vijijini mkoani Ruvuma.

Mwili wa marehemu huyo umekutwa na majeraha ambapo alichomwa kisu mara tatu tumboni kisha kufariki dunia.

ASKARI SONGEA WAJERUHIWA NA KITU KINACHODAIWA KUWA NI BOMU LA KURUSHWA NA MKONO



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

ASKARI watatu  wa Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, wamelazwa katika hospitali ya mkoa huo iliyopo Songea mjini  wakiwa wanapatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu la kurusha kwa mkono.

Tukio hilo limetokea Septemba 16 mwaka huu majira ya jioni katika kata ya Msufini mjini hapa, ambapo wamejeruhiwa.

Akizungumzia tukio hilo kaimu kamanda wa polisi wa mkoa huo ASP George Chiposi,  alisema kuwa watu watatu wasio fahamika ndio waliotupa kitu hicho kinacho sadikiwa kuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono.

Bomu hilo alisema limetengenezwa kienyeji na kuwajeruhi askari  hao watatu waliokuwa doria.

Wednesday, September 10, 2014

SERIKALI YARUHUSU WAFANYABIASHARA KUUZA MAHINDI NJE YA NCHI



Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

SERIKALI hapa nchini imeruhusu wafanyabiashara kuuza mahindi yao nje ya nchi popote pale, huku ikiwataka kuzingatia bei elekezi iliyowekwa ili kumfanya mkulima asiweze kupata hasara.

Sambamba na hilo mahindi ambayo yamehifadhiwa katika vituo husika vilivyopo mkoani humo, serikali itayanunua kwa kilo shilingi 500 na kwamba wakulima hawaruhusiwi kuingiza mahindi mengine katika vituo.

BASI LA SUPER FEO LAPATA AJALI LEO WATATU WAFARIKI DUNIA 25 WAJERUHIWA VIBAYA



 



Picha hizi zinaonesha basi lenye namba za usajili T 273 CDD mali ya kampuni ya Super Feo lililopata ajali katika kijiji cha Sanangula mkoani Ruvuma, ambalo lilikuwa likisafiri leo kutoka Songea mjini kwenda mkoani Mbeya.
 


Na Kassian Nyandindi,

Songea.

WATU watatu wamefariki dunia na wengine 25 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Songea mjini mkoani Ruvuma, kwenda  jijini Mbeya kumgonga mwendesha baiskeli na baadaye kupinduka.

Habari zilizopatikana leo mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela amesema kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 4:45 asubuhi, katika eneo la Sanangula nje kidogo ya Manispaa ya songea mkoani humo.

Kamanda Msikhela amefafanua kuwa ajali hiyo imetokea kwenye barabara ya kutoka Songea kwenda Njombe, ambapo namba za gari yenye usajili T273 CDD aina ya Mitsubishi Rosa mali ya kampuni ya Super feo mjini Songea ambalo lilikuwa linatoka Songea kwenda Mbeya.

Tuesday, September 9, 2014

MKUU WA WILAYA MBINGA AWA MBOGO, AWASHUKIA WAFANYABIASHARA WA KAHAWA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewashukia wafanyabishara wenye tabia ya kutorosha kahawa wilayani humo kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja, na atakaye endelea kufanya hivyo pale atakapobainika atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kunyang’anywa kibali cha ununuzi wa zao hilo wilayani humo.

Alitoa onyo hilo wakati alipokuwa akifunga kikao cha wadau wa kahawa kanda ya Ruvuma, kilichofanyika katika ukumbi wa Jimbo Katoliki mjini hapa.

WATAKIWA KUZALISHA MICHE YA KAHAWA KWA WINGI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKURUGENZI mkuu wa bodi ya kahawa Tanzania (TCB) Adolf  Kumburu ameziasa Halmashauri na taasisi mbalimbali hapa nchini ambako zao la kahawa linazalishwa, kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika kuzalisha miche bora ya kahawa ili kuweza kuwafikia wakulima walio wengi kiurahisi na kukua kwa uzalishaji wa zao hilo.

Alisema pamoja na Taasisi ya utafiti wa kahawa nchini (TaCRI) kuzalisha miche hiyo na kuisambaza, bado haitoshelezi mahitaji, kutokana na uzalishaji kuwa mdogo hivyo ili kuondokana na tatizo hilo wakulima, halmashauri na taasisi zingine zinapaswa kushiriki katika kuanzisha bustani mama za kuzalishia miche ya kahawa.

Saturday, August 30, 2014

OFISA USHIRIKA MBINGA AONJA JOTO YA JIWE, WANACHAMA WAMKATAA WASEMA HAWANA IMANI NAYE


Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

OFISA ushirika wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Raphael Luvanda amejikuta akiwa katika wakati mgumu kufuatia Wanachama wa chama cha kuweka na kukopa, Mbinga Lutheran SACCOS kilichopo wilayani humo kumjia juu na kumweleza kwamba hawana imani naye katika utendaji wa kazi zake, hivyo hawamtaki kumuona akifanya kazi za ukaguzi katika umoja huo.

Sambamba na hilo wanachama hao ambao walionekana kukerwa na tabia za Ofisa ushirika huyo walisema, sababu zao za msingi za kumkataa wamekuwa wakimtuhumu kwa muda mrefu kwamba anafanya kazi zake kwa mrengo wa kushoto kwa kutofuata taratibu husika.

Walieleza kuwa bodi husika itazifikisha tuhuma husika kwa mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga, ili ziweze kufanyiwa kazi huku wakitaka kuanzia sasa shughuli za ukaguzi zifanywe na ofisa ushirika mwingine kutoka katika halmashauri hiyo na sio vinginevyo.

BODI YA LESENI YA GHALA YATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE IPASAVYO



Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

WADAU wanaozalisha mazao ya chakula na biashara wilayani Mbinga na Nyasa mkoa wa Ruvuma, wameitaka bodi ya leseni ya ghala Tanzania kuhakikisha kwamba wanatekeleza mapema mfumo wa stakabadhi ghalani hususani kwa zao la kahawa, ili kuweza kuzuia uharibifu na upotevu wa mazao wilayani humo.

Walisema lengo la kufanya hivyo itasaidia walengwa wa mfumo huo ambao ni wakulima, wafanyabiashara na vikundi husika kuweza kujijengea uwezo na hatimaye waweze kuinua uchumi wao.

Ilielezwa kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani endapo utatekelezwa kwa haraka katika wilaya hizo, utaleta fursa ya kufanyika kwa mnada wa zao la kahawa na kuuzwa katika kipindi hiki cha msimu wa mavuno ya zao hilo.

Friday, August 22, 2014

VIONGOZI WAPYA CHADEMA MBINGA WAPEWA SOMO


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kimepata viongozi wapya ambao watakiongoza chama hicho wilayani humo baada ya kufanya uchaguzi wake, huku wakitakiwa kufanya kazi bila ubaguzi au upendeleo wa aina yoyote ile.

Aidha viongozi hao waliochaguliwa wameshauriwa kutojenga makundi katika kipindi cha uongozi wao ikiwa ni lengo la kuondoa mipasuko ndani ya chama ambayo inasababisha malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Hayo yalibainishwa na Wajumbe wa mkutano Mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa CHADEMA ngazi ya wilaya ya Mbinga, uliofanyika kwenye ukumbi wa Tulivu uliopo mjini hapa.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mwakilishi wa chama hicho Kanda ya kusini Menlufu Mapunda, ambapo wajumbe hao kwa nyakati tofauti walisema itakuwa ni jambo la kusikitisha endapo watawaona viongozi wao wakiwatenga katika mambo mbalimbali, huku wakisisitiza ni vyema kuanzia sasa pawepo na mabadiliko chanya ambayo yataleta maendeleo kwa wanachama na chama kwa ujumla.

Saturday, August 16, 2014

WALEMAVU NAMTUMBO WAPATIWA MAFUNZO YA KUTAMBUA HAKI ZAO

Na Kassian Nyandindi,


Namtumbo.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la kuendeleza watu wenye ulemavu na watoto yatima Tanzania (SHIKUWATA) lenye makao yake makuu mkoani Ruvuma, limeendesha mafunzo ya siku tano kwa watu wenye ulemavu na Watendaji wa kata ya Namabengo Wilayani Namtumbo mkoani humo, kwa lengo la kuwafundisha juu ya kujua sera ya maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu.

Mafunzo hayo ambayo yalifunguliwa na Diwani wa kata ya Namabengo wilayani humo Vitus Ngonyani, ambayo yalifanyika katika ukumbi wa Namabengo Saccos uliopo mjini hapa na kushirikisha wananchi mbalimbali wanaoishi kuzunguka eneo la kata hiyo.

Mratibu wa shirika hilo Laura Martin akizungumza katika mafunzo hayo, alisema kuwa lengo la kutoa elimu kwa walemavu hao ni kuwafanya wajue haki zao na wajibu wa kujihudumia pamoja na kuangalia nafasi waliyonayo katika jamii na serikali kwa ujumla.

Laura alisema kuwa washiriki hao katika kipindi chote cha siku tano watakachokuwa darasani wataweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kujua hali ya watu wenye ulemavu, huduma za watu wenye ulemavu, haki na ulinzi wa kisheria, dira na mwelekeo wa sera, matamko ya sera kwa watu wenye ulemavu na mgawanyo wa majukumu katika ulinzi na usalama kwa watu wenye ulemavu.

Friday, August 15, 2014

ASKOFU MKUU DAMIAN DALLU AWAASA WAUMINI WAKE

Watoto wa shirika la kipapa (mtoto Yesu) parokia ya Mbangamao Jimbo la Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakisherehekea siku ya maadhimisho ya miaka 50 ya uinjilishaji wa parokia hiyo. Sherehe hizo zilifanyika nje ya viwanja vya kanisa hilo.

Askofu mkuu Damian Dallu wakati akitoa mahubiri katika maadhimisho hayo kwa waumini wa kanisa Katoliki (hawapo pichani) Parokia ya Mbangamao Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma. (Picha zote na Julius Konala)

Na Julius Konala,
Mbinga.

ASKOFU mkuu Damian Dallu, wa Jimbo kuu Katoliki la Songea mkoani Ruvuma ameipongeza Parokia ya Mbangamao iliyopo katika Jimbo la Mbinga mkoani humo, kwa mchango wake mkubwa wa kusukuma maendeleo hususani katika sekta ya elimu kwa kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964 chini ya Paroko wake wa kwanza mzalendo Hayati Askofu Maurus Komba.

Askofu Dallu ametoa pongezi hizo wakati akiwahubiria mamia ya Waumini wa kanisa hilo kwenye maadhimisho ya Ibada ya misa takatifu ya shukrani, Jubilei ya miaka 50 ya parokia hiyo iliyofanyika nje ya viwanja vya kanisa hilo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo maaskofu, mapadre, watawa, waumini pamoja na viongozi wa serikali.

Alisema Parokia hiyo kupitia Shirika la Wavisenti imefanikiwa kupanua wigo mkubwa wa kutoa huduma kwa jamii, ikiwemo kuongeza idadi ya shule za msingi hadi kufikia 15, shule za sekondari tatu na ujenzi wa shule za chekechea kwa kila kigango.

Vilevile ameeleza kuwa wameweza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo ikiwemo pamoja na parokia hiyo kuzaa parokia mpya ya Mpepai iliyopo wilayani humo na kufanya ukarabati wa zahanati, shule za msingi na ujenzi wa sekondari. 

WAFANYABIASHARA WA MAHINDI RUVUMA WALIA NA SERIKALI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

BAADHI ya Wasafirishaji wa mazao ya nafaka mkoani Ruvuma, wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuharakisha kulipa madeni yao ya usafirishaji wa mahindi kutoka kwenye vituo vya ununuzi na kuyafikisha kwenye kitengo cha hifadhi ya chakula (NFRA) Songea mkoani humo, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2013/2014 kwa lengo la kunusuru kuuziwa mali zao na taasisi za kifedha ambako walikopa kwa ajili ya kuendeshea shughuli hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasafirishaji hao ambao ni wazawa hawakutaka majina yao yatajwe, walidai kwamba hali hiyo imewaathiri zaidi  waajiriwa waliopitia mgongo wa nyuma kufanya kazi ya usafirishaji wa zao hilo baada ya matajiri wao kuingia mkataba na NFRA.

Walisema kuwa tangu kufunguliwa kwa msimu huo Julai 15 mwaka jana wamekuwa wakiendesha shughuli hizo kwa kutegemea mikopo kutoka benki, na wengine kudaiwa na baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta ambako walikopa.

Tuesday, August 12, 2014

WANASIASA WANYOSHEWA KIDOLE KWA KUWATUMIA VIJANA KATIKA USHABIKI WA MAMBO YA KISIASA

Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea mjini mkoani Ruvuma, Josephat Ndulango. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,

Songea.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mjini mkoani Ruvuma kimewanyoshea kidole wanasiasa ambao wamekuwa wakiwatumia vijana kwa maslahi yao binafsi, kupitia mchakato huu wa kutengeneza katiba mpya unaoendelea huko Bungeni badala yake kimewataka waachane na ushabiki wa mambo ya kisiasa, na wawatumie vijana kwa maslahi ya taifa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha imeelezwa kuwa utengenezaji wa katiba mpya ni jukumu la Wabunge wa bunge maalum la katiba, hivyo kwa wale waliokimbia mapambano bungeni ni kutowatendea haki wananchi na ni dhambi ambayo itaendelea kuwatafuna kila siku maishani mwao, badala yake warudi bungeni ili kuweza kumaliza misuguano inayoendelea kufukuta na kuhatarisha ustawi wa maendeleo ya nchi yetu.

Katibu wa CCM wilaya ya Songea mjini, Josephat Ndulango alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Majira mjini hapa, huku akieleza kuwa vyama vya upinzani ndio vimekuwa chagizo kwa kukataa kujenga maridhiano ya pamoja juu ya mchakato huo wa kuipata katiba mpya.

Saturday, August 9, 2014

ASILMIA 90 YA FAMILIA WILAYANI MBINGA HUTEGEMEA KILIMO NA UFUGAJI

Upande wa kulia Diwani wa kata ya mkako Ambrose Nchimbi akiangalia nyara mbalimbali za serikali katika banda la Maliasili na mazingira wilayani Mbinga, siku ya maonesho ya wakulima yaliyofanyika katika kilele chake kijiji cha Lusonga wilayani humo.

Mke wa Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, Leah Kayombo akitoa maelezo juu ya shughuli zinazofanywa na umoja wa kikundi cha Mbalawala katika maonesho ya wakulima yaliyofanyika wilayani Mbinga katika kijiji cha Lusonga mkoani humo.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa asilimia 90 ya familia wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, hutegemea kilimo na ufugaji katika kuendesha shughuli za kimaendeleo katika maisha yao ya kila siku.

Aidha kati ya hizo asilimia 50 zinazalisha zao la kahawa wilayani humo, na ndio zao kuu ambalo hutegemewa kwa kukuza uchumi wa wilaya hiyo.

Hayo yalisemwa na Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mbinga, Oscar Yaspesa alipokuwa akisoma taarifa ya maendeleo ya kilimo na mifugo kwa mgeni rasmi Diwani wa kata ya Mkako Ambrose Nchimbi alipokuwa kwenye maonesho ya wakulima (Nane nane) yaliyofanyika katika kijiji cha Lusonga wilayani humo.