Na Muhidin Amri,
Madaba.
KITENDO kilichofanywa cha kukarabati kituo
cha Mabasi ya abiria Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma,
kimepongezwa huku baadhi ya abiria na wamiliki wa magari yanayobeba abiria hao wakiuomba
uongozi wa halmashauri hiyo, kuongeza changarawe katika maeneo ambayo magari
yanasimama katika kituo hicho.
Ombi hilo lilitolewa juzi kwa nyakati
tofauti wakati abiria hao na watumiaji wengine wa kituo hicho walipokuwa
wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari.
Walisema kuwa kazi iliyofanywa ya
kukarabati miundombinu ya kituo hicho ni nzuri, lakini wanaomba katika maeneo
ambayo magari yanasimama ziongezwe changarawe ili kuondoa hali ya utelezi
ambayo hutokea hasa kipindi hiki cha masika.
Madereva wa magari ya abiria
walipongeza hatua iliyochukuliwa na uongozi wa halmashauri hiyo walisema kazi
iliyofanywa hapo ni nzuri, ambapo Erick Malecela ambaye ni dereva wa basi la
abiria linalofanya safari zake kati ya mkoa jirani wa Njombe na Songea kupitia
Madaba alisema, ukarabati huo umesaidia kushawishi madereva wengi kuingia na
kutoka kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria.
“Bado tatizo ni utelezi kwa baadhi ya
maeneo kwani pindi mvua zinaponyesha tunapata tabu tunaiomba halmashauri kuangalia
uwezekano wa kumwaga changarawe, badala ya kutumia udongo ambao sio rafiki sana
ya maji hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha katika maeneo
mengi”, walisema.
Pia Kituo hicho cha magari ya abiria ndicho
ambacho kinategemewa kuwa ndiyo chanzo kikuu kimojawapo cha kuingiza mapato ndani
ya halmashauri hiyo.
Andrew Msigwa ambaye ni mkusanyaji wa
ushuru katika kituo hicho mbali na kuishukuru halmashauri kwa kazi ya ukarabati
huo, ameliomba Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kuhakikisha linachukua
hatua kwa madereva wa mabasi ya abiria ambao wanakaidi kuingia ndani ya kituo wakati
wa kushusha na kupakia abiria.
Alisema kuwa wapo baadhi ya madereva
wasumbusu ambao hawataki kuingia kituoni hapo, jambo ambalo linasababisha
halmashauri kukosa mapato yake ikiwemo fedha ambazo zingeweza kusaidia
marekebisho mengine madogo madogo.
Mweka hazina wa halmashauri ya wilaya
ya Madaba, Emmanuel Abraham alibainisha kuwa mpango uliopo wa halmashauri hiyo katika
bajeti yake ya mwaka 2018/2019 ni kuhakikisha kwamba inaweka tabaka la lami katika
kituo hicho, na kukamilisha ujenzi wa miundombinu yote muhimu inayohitajika ili
watumiaji wa kituo hicho waweze kupata huduma zote za msingi ikiwemo kukamilisha
ujenzi wa vibanda vya biashara vinavyozunguka kituo hicho.
No comments:
Post a Comment