Juma Homera, Mkuu wa wilaya ya Tunduru. |
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
BAADHI ya wakazi wilayani Tunduru mkoa
wa Ruvuma wameipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa hatua ya kumaliza
ujenzi wa barabara ya kutoka Namtumbo hadi Tunduru mkoani humo kwa kiwango cha
lami.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti
na mwandishi wetu Alli Mrope, Kassim Kassim na Rashid Uledi walisema kuwa kukamilika
kwa barabara hiyo ni hatua moja mbele ya kuharakisha maendeleo ya wananchi wa
wilaya hiyo.
Mrope alisema kuwa mbali na kuishukuru
Serikali kwa ujenzi huo ameiomba pia kuendelea na mikakati ya kutekeleza miradi
mingine ya maendeleo ambayo itasaidia kuharakikisha kukua kwa uchumi.
Alisema kuwa wilaya ya Tunduru ni
kati ya wilaya ambazo zina rasilimali
nyingi hapa nchini, hata hivyo bado haijaweza kutumika vyema kutokana na
kuchelewa kukamilika kwa miundombinu ya barabara na nishati ya umeme ambayo ni
muhimu katika suala la kukua kwa uchumi.
Vilevile ameitaka Serikali kuangalia
maeneo mengine ikiwemo huduma ya nishati ya umeme ambayo ni tatizo kubwa kwa
wilaya hiyo kwa sababu itachelewesha mpango wa Serikali wa uanzishwaji wa
viwanda.
Kassim alisema kuwa kukamilika kwa
barabara ya lami kutoka Namtumbo Tunduru hadi Mang’aka mkoa jirani wa Mtwara ni
jambo la faraja ambalo wananchi wa Tunduru wataendelea kuishukuru Serikali yao
kwa kuwa muda mrefu barabara hiyo ilikuwa kikwazo kikubwa katika kupambana na
umaskini.
Naye Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma
Homera alisema Serikali imedhamiria kwa dhati kumaliza changamoto zote ikiwemo
suala la umeme kwani tayari imeshaanza kusambaza nishati hiyo kwa baadhi ya vijiji
kupitia mradi wa umeme vijijini REA.
Homera alisema tayari baadhi ya
vijiji katika jimbo la Tunduru kusini vimeshapata umeme na kwamba REA imejipanga
kuhakikisha kuwa vijiji vyote vya wilaya hiyo vinapata umeme haraka
iwezekanavyo na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati huu ambao utekelezaji
wake unafanyika.
No comments:
Post a Comment