Na Dustan Ndunguru,
Songea.
NAIBU Katibu Mkuu mstaafu wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mwigulu Nchemba amewataka wanachama wa Chama hicho jimbo
la Songea mjini Mkoani Ruvuma, kuvunja makundi yaliyojitokeza wakati wa
mchakato wa kura za maoni ili kuweza kukirahisishia ushindi CCM katika uchaguzi
mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 13 mwaka huu.
Pia amewataka wananchi wa jimbo hilo
kutofanya makosa kupigia kura upinzani kwani kitendo hicho huenda kikasababisha
maendeleo waliyofikia kudumazwa kutokana na kudaiwa kuwa na uwezo mdogo wa
kuongoza walionao baadhi ya viongozi wa kutoka kambi pinzani.
Mwigulu alisema hayo jana alipokuwa
kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Ubunge uliofanyika kwenye
viwanja vya Kibulang’oma kata ya Lizaboni mjini hapa.
Kampeni hizo zilihudhuriwa na wanachama
wa Chama cha mapinduzi wakiwemo na viongozi mbalimbali na wananchi.
Alisema kuwa wakati wa mchakato wa
kura za maoni katika jimbo hilo walijitokeza wanachama 20 kuomba nafasi hiyo, hivyo
ni dhahiri kulikuwa na makundi sawa ambayo hivi sasa yanapaswa kuungana pamoja ili
kukipa ushindi chama hicho kwa kumnadi kwa nguvu zote mgombea Dokta Damas
Ndumbaro.
Alisema kuwa kama makundi ndani ya
chama hayatatoweka kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kutoa mwanya kwa wapinzani
kushinda jambo ambalo halipaswi kupewa nafasi katika jimbo hilo na kwamba CCM
ndicho chama pekee chenye dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi wake maendeleo
kutokana na kuwa na sera nzuri zisizokuwa na ubaguzi.
Naye mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa
tiketi ya Chama hicho, Dokta Ndumbaro aliomba kura kwa kusema kuwa endapo
atachaguliwa kuongoza jimbo hilo atahakikisha anatekeleza kwa vitendo yale yote
ambayo yaliahidiwa na mtangulizi wake marehemu Leonidas Gama na kwamba
anafahamu wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinapaswa
kupatiwa ufumbuzi ikiwemo elimu, barabara, maji, afya na soko la mazao yao.
Dokta Ndumbaro alisema kuwa changamoto
zilizopo kwenye sekta ya kilimo hususan masoko ya mazao ya wakulima chama pekee
kinachoweza kutatua kero hizo ni CCM.
No comments:
Post a Comment