Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WITO umetolewa kwa Viongozi wa
taasisi za Serikali na binafsi mkoani Ruvuma, kuwa karibu na Waandishi wa
habari pale wanapohitaji ufafanuzi wa mambo muhimu ya maendeleo kwa faida ya
wananchi, ikiwemo kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha imeelezwa kuwa viongozi hao
waache tabia ya kumwona mwandishi wa habari kama adui, badala yake wanapaswa kuona
ni marafiki na kutoa ushirikiano wa kutosha katika kazi zao za kila siku.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christine
Mndeme alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa
mkoa huo katika Ikulu ndogo mjini Songea.
Alisema kuwa kumkwepa mwandishi wa
habari ni kitendo ambacho hakikubaliki katika jamii na kwamba aliongeza kuwa,
hategemei kusikia hasa kwa wakuu wa taasisi za Serikali mkoani humo wakifanya vitendo
vya kutoshirikiana na waandishi hao katika kujenga maendeleo ya mkoa na taifa kwa
ujumla.
“Niwapongeze wale mnaoibua maovu sisi
Serikali tupo tayari kuyafanyia kazi, Ofisi yangu ipo wazi muda mwingi
nawakaribisheni mje tushirikiane katika kuutangaza mkoa wetu, ili malengo ya
Serikali ya awamu ya tano yaweze kuwafikia ipasavyo wananchi wake”, alisema.
Vilevile aliwataka wanahabari kuwa
karibu na jamii katika kuisaidia Serikali kuibua changamoto mbalimbali
zinazowakabili wananchi.
Alisisitiza kuwa wanahabari katika
mkoa huo wanapaswa kufuata maadili yao ya taaluma kwa kuzingatia uaminifu,
weledi na uzalendo na kuwa tayari kujituma sehemu yoyote ile pasipo kuvunja
sheria za nchi.
“Tunapoandika habari zetu basi tuuvae
uzalendo zaidi kwa sababu amani, utulivu na maendeleo tuliyonayo ni yetu sote
tukiharibu ni sisi tutakuwa tumeharibu kalamu yetu, mkono wetu na macho yetu
isiwe ni chanzo cha upotoshaji katika kufanya kazi zetu za kila siku na pia
tujiepusha na watu wenye nia mbaya ambao huwatumia ninyi waandishi kwa namna
moja au nyingine kupotosha umma kwa maslahi yao binafsi”, alisisitiza Mndeme.
No comments:
Post a Comment