Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
MKURUGENZI wa vijana jimbo katoliki
la Mbinga mkoani Ruvuma, Padri Donatus Komba amewataka vijana kuacha tabia ya
kukaa vijiweni bila kufanya kazi, badala yake wajiunge pamoja na kuanzisha
vikundi vya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Padri Komba ambaye pia ni Paroko wa
Parokia ya Kindimba alisema hayo wakati alipokuwa akihubiri katika kanisa hilo
hivi karibuni na kusema kuwa, kitendo kinachofanywa na vijana kukaa na kucheza
kamali vijiweni katika kijiji cha Kindimba kinapaswa kukemewa kwa nguvu zote
ili kuwanusuru wasiharibikiwe katika maisha yao.
Alisema kuwa vijana ni kundi
linalotegemewa katika kuendeleza taifa lolote lile kwa mustakabali wa maendeleo
husika hivyo wazazi na walezi wanakila sababu ya kuhakikisha wanatoa maelekezo
yaliyosahihi kwa watoto wao ili wasijiingize kwenye vitendo viovu.
Padri huyo alifafanua kuwa mchezo wa
kamali ambao umeshamiri katika kijiji hicho umesababisha kushamiri kwa vitendo
vya wizi ambavyo vimekuwa vikisababisha wananchi kuibiwa katika maeneo
mbalimbali kijijini humo na kwamba viongozi wanakilasababu ya kuhakikisha
wanawaelekeza vijana wao juu ya umuhimu wa kujikita katika shughuli za
uzalishaji mali.
“Vijana hawa wacheza kamali wamekuwa
wakikusanyika katika kijiji hiki kutoka vijiji jirani vya Mahenge, Unango, Mkumbi,
Litembo na Mundeki”, alisema Komba.
Alisema kuwa pamoja na kucheza mchezo
wa kamali pia vijana hao hujiingiza kwenye vitendo vya utumiaji wa madawa ya
kulevya ikiwemo uvutaji wa bangi hali ambayo huchangia kudhoofisha nguvu kazi
hii muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Aliwataka wazazi, viongozi wa Serikali
na wanasiasa kushirikiana pamoja kukemea jambo hili linaloendelea kukua kwa
kasi katika kijiji hicho na kwamba, wakati umefika kwa vijana kujikita katika
shughuli za kilimo ambacho kimsingi kama watafanya hivyo hawatakuwa na muda kwa
kupoteza wa kukaa vijiweni.
Mkurugenzi huyo wa vijana pia
aliwaasa vijana kujiunga na vyuo vya ufundi ambavyo vimekuwa vikitoa kozi
mbalimbali ili hatimaye waweze kupata ujuzi ambao mwisho wa siku watakuwa na
uwezo wa kujiajiri wao wenyewe au kuajiriwa.
No comments:
Post a Comment