Azory Gwanda. |
MWENYEKITI wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga amelitaka jeshi la Polisi nchini
kufanya uchunguzi wake kwa haraka ili kuwezesha kupatikana kwa Mwandishi wa
habari wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Azory Gwanda.
Azory ametoweka siku ya 18 sasa huko
Kibiti ambako anaishi na familia yake.
Akizungumza na Mwandishi wetu baada
ya kufungua kongamano la maadhimisho ya siku ya haki za binadamu leo Ijumaa,
Nyanduga alisema kuwa kupotea kwa mwandishi huyo kuna viashiria vya uvunjifu wa
haki za binadamu.
“Matukio haya sasa yamekuwa mengi na yameanza
kuzoeleka, tunaliomba jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wake haraka ili
mwandishi huyu apatikane”, alisema Nyanduga.
Alisisitiza kuwa kila mtu anao wajibu
wa kulinda haki za binadamu lakini Serikali ndiyo ina wajibu mkubwa kwa sababu
ina wajibu wa kulinda maisha ya watu wake.
Nyanduga alibainisha kuwa tume yake
inalaani vitendo vyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu na mara nyingi
wanaunda kamati kwa ajili ya kuchunguza matukio hayo na kutoa ripoti.
No comments:
Post a Comment