Na Muhidin Amri,
Tunduru.
KAIMU Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chiza Malando amemsimamisha
kazi Mtendaji wa kijiji cha Chilundundu wilayani humo, Timamu Issa kwa tuhuma
ya kutengeneza mbinu chafu ya kutafuna mamilioni ya fedha za Mpango wa kunusuru
kaya maskini (TASAF) katika kijiji hicho.
Sambamba na kumsimamisha kazi mtendaji
huyo, Mkurungezi huyo amevunja kamati ya watu 14 ambayo ilikuwa ikisimamia
utekelezaji wa mpango huo.
Malando alilazimika kuchukua hatua
hiyo wakati alipokuwa akizungumza juzi na wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) katika ukumbi wa Chama cha ushirika, Chiliwena Amcos ikiwa ni
siku chache tu baada ya mbinu za viongozi hao kutaka kutafuna fedha hizo kubainika
na wataalamu wa wilaya hiyo.
Alisema kuwa maamuzi hayo ameyachukua
baada ya viongozi hao kubainika pia kutaka kuwaibia wanufaika wapatao 132
katika kijiji hicho zaidi ya shilingi milioni 1.8 ambazo zilipangwa kulipwa kwa
wanufaika wa mpango huo.
Kufutia uwepo wa hali hiyo, Malando
aliwataka walengwa wa mpango kufanya uchaguzi upya kwa kuteua wajumbe wapya ambao
wataweza kuongoza kwa kufuata taratibu husika.
Alisema kuwa kulingana na maelekezo
ya utendaji wa Serikali ya awamu ya tano, haiwezekani kuendelea kuwavumilia
viongozi wa mtindo huo ambao wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo ya wananchi wenzao
na kuigombanisha Serikali na wananchi wake.
“Mtendaji huyu asimame kazi kuanzi
leo hii ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili”, alisema.
Malando aliongeza kuwa tume atakayounda
kuchunguza jambo hilo itafanya kazi kwa haraka na ikibainika kuwa ni kweli hatua
kali zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.
Awali akitoa taarifa hiyo Mratibu wa
TASAF wilaya ya Tunduru Emmanuel Luhanzu alisema kuwa njama za kutaka kuiba
fedha hizo ziligundulika wakati wa malipo yaliyofanyika Desemba 5 mwaka huu, baada
ya wasimamizi wa malipo ya mradi huo kutoka katika kijiji hicho (CMC) kuonekana
wakitumia muda mwingi kufanya hesabu za malipo ya mnufaika mmoja.
Alisema baada ya kulibaini hilo
alisogea taratibu hadi katika meza ya kulipia na kubaini uwepo wa karatasi
nyingine nje ya karatasi ambayo ilipelekwa na TASAF wakati wa kuandaa malipo
hayo.
Alisema katika kuhakikisha kuwa
wanafanikisha mbinu za wizi huo zinafanikiwa mtendaji huyo alifika katika kituo
cha malipo hayo akiwa amelewa na kuanzisha vurugu jambo ambalo lilileta
taharuki kwa wanufaika hao.
Naye Mratibu wa mpango huo wilayani hapa,
Muhidin Shaibu aliwahimiza walengwa hao kufanyia kazi haraka maelelekezo
yaliyotolewa na Mkurugenzi mtendaji, Malando kwa kuchagua haraka kamati mpya
ambayo itasimamia kikamilifu ili kuwezesha mpango huo kuweza kuendelea vizuri.
Shaibu alisema kuwa endapo
watashindwa kutekeleza maelekezo hayo upo uwezekano wa kuufuta mradi huo katika
kijiji chao na kupelekwa katika vijiji vingine na kwamba Mfuko huo wa maendeleo
ya jamii unatekeleza mradi huo katika vijiji 88 tu wilayani Tunduru na kwamba vijiji
vingine 66 havijapelekewa mradi huo.
No comments:
Post a Comment