Na Muhidin Amri,
Mbinga.
BAADHI ya Wananchi wa Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wameitaka
Halmashauri ya mji huo kuongeza kasi katika suala la kufanya usafi wa mazingira
ili kuweza kuepusha uwezekano wa kutokea magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwemo
kipindupindu hasa kipindi hiki cha masika.
Walisema kuwa kwa muda mrefu halmashauri hiyo imekuwa
ikisuasua katika masuala ya utekelezaji wa usafi wa mazingira ya mji huo katika
maeneo mbalimbali, huku watendaji wake wenye dhamana wakiona mlundikano wa
uchafu mitaani na kushindwa kuchukua hatua madhubuti ya kumaliza tatizo hilo.
John Mapunda ambaye ni mkazi wa mtaa wa Kipika alisema kuwa kipindi
hiki ni cha masika na ndiyo muda ambao hatari zaidi kwa magonjwa ya mlipuko,
hivyo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Robert Kadaso Mageni kwa
kushirikiana na wataalamu wake wa masuala ya usafi wa mji huo wanapaswa
kuchukua hatua madhubuti ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea hapo baadaye.
Alisema mji wa Mbinga ni mdogo lakini uzalishaji wa
taka umekuwa mkubwa kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu hasa wafanyabiashara
ndogondogo na mama lishe ambao wamekuwa wakitupa taka hovyo na usimamizi wa
kudhibiti tatizo hilo mitaani umekuwa mdogo.
Ester Komba alisema hata uchafu unaotupwa kwenye maghuba bado
ni tatizo kubwa kwa sababu umekuwa ukikaa kwa muda mrefu bila kuzolewa na
kufikia hatua ya kuoza na kutoa harufu na kuwa kero kwa wananchi.
Komba alisema kuwa wanamsubiri kwa hamu kubwa Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa ili wamueleza kero hiyo na matatizo mengine yanayoendelea kuwa
kero kwao na yanaonekana baadhi ya viongozi wa mji huo muda mwingi kujali
maslahi yao binafsi badala ya kuwatumikia wananchi.
Alisema kuwa ni aibu kubwa mji wa Mbinga ambao una wananchi wenye
nguvu kubwa ya kiuchumi kuwa mchafu jambo ambalo linaonesha kuwa hata
Mkurugenzi wake anayeongoza mji huo kushindwa kusimamia kikamilifu baadhi ya majukumu
aliyopewa na Serikali.
Hata hivyo jitihada za mwandishi wa habari hizi alipomtafuta
Mkurugenzi mtendaji wa mji wa Mbinga, Robert Kadaso Mageni ili aweze kutolea
ufafanuzi wa kero hiyo hakuweza kupatikana Ofisini kwake na pale alipopigiwa
simu ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment