Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha
Mkumbi kata ya Mkumbi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamejitokeza na
kushirikiana pamoja kujenga shule ya msingi Magingo iliyopo kwenye kata hiyo ikiwa
ni jitihada yao na lengo la kuwaondolea adha wanayoipata hivi sasa watoto wao
kwenda kusoma umbali mrefu.
Aidha imefafanuliwa kuwa ujenzi wa
shule hiyo unatokana pia na watoto wanaosoma katika shule ya msingi Lugari
katika kata hiyo kuwa wengi na vyumba vya madarasa havitoshelezi.
Benuard Komba ambaye ni Mwenyekiti wa
kijiji hicho alisema kuwa ujenzi huo ni muunganiko wa nguvu za wananchi kwa
lengo la kuweza kumaliza changamoto wanayoipata watoto wao kutembea umbali mrefu
wa kilometa mbili kufuata elimu.
Alisema kuwa katika kipindi cha
masika wanafunzi wamekuwa wakipata shida kutembea kwa miguu kwenda shuleni
hivyo waliona ni vyema katika kumaliza kero hiyo wajenge shule nyingine karibu
na makazi yao ili watoto waweze kupata elimu kwa urahisi.
“Tuliona ni vyema kujenga shule hii,
watoto darasani wanakuwa zaidi ya 100 tunajenga tuweze pia kupunguza wingi wa
watoto kurundikana darasani na kumrahisishia hata mwalimu anapokuwa kwenye
vipindi vya masomo aweze kufundisha kwa urahisi”, alisema Komba.
Ujenzi wa shule hiyo ambao ulianza
Agosti 21 mwaka huu hivi sasa tayari wameweza kufikia hatua ya kukamilisha
jengo moja lenye vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu.
Vilevile mwandishi wetu ameshuhudia
ujenzi wa jengo la pili ukianza huku taratibu za ujenzi wa vyoo na nyumba za
walimu ukiendelea kufanyika ambapo mara ujenzi huo utakapokamilika ikifikapo
Januari mwaka huu wanatarajia watoto waweze kuanza kusoma katika majengo hayo.
Naye Gabinus Kapinga ambaye ni
mwananchi wa kijiji cha Mkumbi alisema kuwa wanaiomba Serikali iendelee
kuwaunga mkono ili waweze kufikia hatua nzuri ya kuweza kukamilisha haraka
ujenzi wa majengo hayo na watoto wao waweze kusoma mahali pa zuri.
Kadhalika akizungumzia hilo Kaimu
Afisa mipango wa wilaya ya Mbinga, Zainabu Mfinanga alieleza kuwa ujenzi huo wanashirikiana
na halmashauri ya wilaya hiyo, ambapo wamekuwa wakiwapatia vifaa vya kiwandani
ili kuweza kufikia hatua nzuri ya kukamilisha kazi hiyo ya ujenzi.
No comments:
Post a Comment