Na Muhidin Amri,
Madaba.
WAKAZI 2,196 wanaoishi katika kijiji
cha Mahanje kata ya Mahanje Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma,
wanatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji ambao ujenzi wake unagharimiwa na
Serikali, ambapo mara baada ya kukamilika kwake unalenga kumaliza kero ya muda
mrefu ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi hao.
Akizungumza katika eneo la mradi huo
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Shafi Mpenda alisema
Serikali imetoa shilingi milioni 275 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao
ulianza kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu na kwamba utakamilika mwishoni mwa
mwezi Februari mwakani 2018.
Mpenda alisema kuwa hapo awali
wananchi wa kijiji hicho walibuni mradi wao wa maji kwa ajili ya kumaliza kero
ya maji, hata hivyo kutokana na ongezeko la kaya ilisababisha kuwepo kwa upungufu
wa maji na Serikali ikaona ni vyema sasa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha
huduma hiyo ili wananchi wengi waweze kunufaika na hatimaye kuondokana na
kutumia muda wao mwingi kufuata huduma hiyo umbali mrefu.
Kadhalika Mkurugenzi huyo alimshukuru
Rais Dokta John Magufuli kwa uamuzi wake wa kutoa fedha hizo za kutekeleza
mradi huo ambao utamaliza kero ya muda mrefu ya maji kwa wakazi wa kijiji cha
Mahanje na maeneo mengine jirani na kijiji hicho.
Mpenda amemuagiza mkandarasi
anayejenga mradi huo Kampuni ya Kipera Construction Company Limited ya kutoka Songea,
kuhakikisha kwamba inafanya kazi usiku na mchana ili kuweza kukamilisha mradi
kwa wakati na sio vinginevyo.
Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi
huo, David Alli aliongeza kuwa kazi hiyo wanatarajia kuikamilisha baada ya
mwezi mmoja kuanzia sasa kwani tayari wamekwisha tega mabomba kutoka kwenye
tenki kubwa hadi kwenye chanzo cha maji.
No comments:
Post a Comment