Na Dustan Ndunguru,
Songea.
Songea.
NAIBU Waziri wa kilimo Dokta Mary
Mwanjelwa amewataka wakulima na wafanyabiashara mkoani Ruvuma,
kuchangamkia fursa ya kufunguka kwa mipaka kwa ajili ya kusafirisha mazao yao
hususan mahindi ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia kanuni na sheria
zilizowekwa na Serikali.
Dokta Mary alisema hayo hivi karibuni
wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika, wakulima
na maofisa ugani katika viwanja vya kituo cha ununuzi wa mahindi (NFRA) Kanda
ya Songea mkoani humo.
Alisema kuwa Serikali katika kuwajali
wakulima wake imeamua kufungua mipaka na kutoa fursa kwa wananchi wake wakiwemo
wakulima, wafanyabiashara na kwa mtu mmoja mmoja kwa lengo la kuwawezesha kwenda
kuuza mahindi yao nchi yeyote yenye uhitaji wa chakula.
Kadhalika aliwaomba wakulima hao
kujiunga kwenye vikundi vya ushirika ili waweze kupata mikopo kwa urahisi
kutoka kwenye taasisi za fedha, kuongeza thamani ya mazao yao ili waweze
kupambana na walanguzi wanaopita kuwalaghai wakulima kwa kununua mazao yao kwa
bei ndogo.
Waziri huyo amepiga pia
marufuku kuuzwa kwa mbolea rejareja na ya kupima katika
mitaa mbalimbali kwa madai kuwa asilimia
kubwa inachakachuliwa na kuwasababishia wakulima kupungua kwa
kiwango cha uzalishaji wa mahindi na kwamba ametoa onyo kwa yeyote atakayekaidi
agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Akiwa mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku
moja Naibu Waziri Mwanjelwa aliweza kutembelea na kukagua maghala ya kuhifadhia
mahindi katika Kituo cha kununulia mahindi (NFRA) Kanda ya Songea pamoja na
eneo la ujenzi wa maghala na vihenge na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mahindi
cha OTC Lilambo kilichopo chini ya Halmashauri ya wilaya ya Songea.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
katika mkutano huo, mmoja wa wakulima hao Isiaka Mapunda alisema kuwa tatizo la
ukosefu wa soko la kuuzia mahindi limesababisha baadhi yao kushindwa kumudu
gharama za kununulia pembejeo za kilimo pamoja na kusomesha vijana wao.
Kwa upande wake John Komba mkulima
kutoka kijiji cha Maposeni wilayani humo alimuomba Naibu Waziri huyo kuona
umuhimu wa kuongeza tani za ununuzi wa mahindi na kuiomba Serikali
kupitia mfuko wa pembejeo wa kilimo kutoa mikopo ya pembejeo hizo kwa wakulima
kwa wakati na riba nafuu.
No comments:
Post a Comment