Monday, December 4, 2017

DED MBINGA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WATU WENYE ULEMAVU

Kikundi cha ngoma kikiburudisha siku ya maadhimisho ya watu wenye ulemavu duniani yaliyofanyika katika kijiji cha Myau kata ya Mbuji wilayani Mbinga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito akisalimiana na mama mmoja ambaye ni mkazi wa kijiji cha Myau kata ya Mbuji mwenye mtoto ambaye ana matatizo ya ngozi (Albino) mara baada ya kumpatia mafuta maalum ya kupaka mtoto huyo ili ngozi yake isiweze kushambuliwa na magonjwa.
Mtoto mwenye matatizo ya ngozi ambaye ni Mkazi wa kijiji cha Myau kata ya Mbuji akipewa mafuta maalum ya kupaka na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito ili ngozi yake isiweze kushambuliwa na magonjwa mbalimbali ambapo mafuta hayo waligawiwa bure siku ya maadhimisho ya watu wenye ulemavu duniani yaliyofanyika katika kijiji cha Myau kata ya Mbuji wilayani hapa.
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gombo Samandito amesema kuwa atashirikiana na wataalamu wake waliopo katika halmashauri hiyo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu.

Aidha alisisitiza kwa kuwataka maafisa maendeleo ya jamii kuhamasisha kundi hilo katika wilaya hiyo kuunda vikundi vya ujasiriamali ambavyo wataweza kuanzisha miradi ambayo itawakwamua kiuchumi.

Samandito alisema hayo juzi wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani wilayani hapa, zilizofanyika katika kijiji cha Myau kata ya Mbuji ambapo sherehe hiyo kitaifa imebeba kauli mbiu isemayo, Badilika tunapoelekea jamii jumuishi na imara kwa wote.


“Ni lazima ifike mahali sasa walemavu wenye uwezo wa kufanya kazi za maendeleo wawezeshwe, ili waweze kuwa chanzo cha mabadiliko katika jamii na kuachana na tabia ya hali waliyonayo kuwa ombaomba”, alisema Samandito.

Alisema kuwa jamii inapaswa kutoa ushirikiano mkubwa kwa watu wenye ulemavu na sio kuwatenga kwani kuna baadhi ya walemavu wanao uwezo wa kufanya kazi na kuingiza kipato kwa faida ya maendeleo ya sasa na baadaye.

Pia alifafanua kuwa maadhimisho hayo ni siku muhimu ambayo inaikumbusha jamii namna ya kuishi pamoja na watu wenye ulemavu na kuwaheshimu kwa kuwapatia haki zote za msingi ambazo wanastahili kuzipata.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya watu wenye ulemavu wilayani Mbinga Mwenyekiti wa Chama Cha Walemavu (CHAWATA) wilayani humo, Martin Mbawala alisema kuwa wilaya hiyo ina jumla ya walemavu 3,246 ambao kati yao wa jinsia ya kiume wapo 1,872 na wa kike ni 1,374.

Mbawala alisema kuwa anaiomba Serikali iendelee na zoezi la uundaji wa mabaraza ya watu wenye ulemavu ili yaweze kufanya kazi ya kutetea haki zao.

Alisema kuwa walemavu wilayani humo wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa viungo bandia, baiskeli (Wheel chair), magongo ya kutembelea, mashine maalum kwa wasiosikia (Viziwi) na kwamba kwa upande wa kundi lenye matatizo ya kuona wanahitaji fimbo nyeupe ili waweze kutembea vizuri.

“Kwa mujibu wa takwimu tulizofanyia utafiti walemavu wanaohitaji viungo bandia wapo 180, baiskeli wapo 300, magongo ya kutembelea wapo 282, wasioona wanaohitaji fimbo nyeupe wapo 180, wasiosikia wanaohitaji kusaidiwa mashine maalum wapo 169 na wenye matatizo ya ngozi wapo 76”, alisema Mbawala.

Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa katika kundi la watu wenye matatizo ya ngozi (Albino) wanahitaji kuendelea kupewa mafuta maalum ya kupaka ili kuweza kuzuia ngozi zao zisiweze kushambuliwa na magonjwa.

No comments: