Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gombo Samandito amesema kuwa zoezi la kusambaza
vifaa vyote vya kiwandani katika miradi ya maendeleo ya wananchi vijijini,
halmashauri hiyo itaendelea kuvisambaza ili kuunga mkono jitihada za maendeleo
zinazofanywa katika jamii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Samandito alisema hayo juzi wakati
alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha
Kibanga na Myau zilizopo katika kata ya Mbuji kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo,
Cosmas Nshenye.
Kadhalika katika kata hiyo
alisisitiza kuleta vifaa vya kiwandani ili kuweza kumalizia ujenzi wa bweni la
kulala wanafunzi katika shule ya Sekondari Mbuji ambayo tayari wananchi wake
wameweza kuonyesha nguvu zao za ujenzi wa jengo hilo.
“Ndugu zangu vifaa vya kiwandani kama
vile nondo, simenti na vinginevyo pale vinapohitajika tuwasiliane ni lazima
tuvilete katika kukamilisha ujenzi wa miradi hii ya wananchi, hivyo naagiza
viongozi wenu waje kuvichukua ili tuweze kufikia malengo yetu tuliyojiwekea
katika kukamilisha miradi hii”, alisisitiza Samandito.
Awali kwa mujibu wa taarifa ya
maendeleo ya wananchi hao juu ya ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Kibanga
na Myau na bweni hilo la kulala wanafunzi katika shule hiyo, inaeleza kuwa
wameweza kuungana pamoja kufyatua tofari, kuchangishana fedha na kuweza kujenga
majengo hayo ambayo sasa yanahitaji nguvu ya Serikali kwa ajili ya kuweza
kupata vifaa vya kiwandani ili yaweze kukamilika ujenzi wake.
Kwa upande wao wananchi hao
walimshukuru Samandito kwa jitihada anazozifanya za kuunga mkono nguvu
hizo za wananchi katika kusambaza vifaa hivyo vya kiwandani katika kuweza
kukamilisha miradi ya maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment