Na Mwandishi wetu,
Madaba.
MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya Wilaya
ya Madaba mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda amewataka wananchi wa Jimbo la Madaba
kuhakikisha kwamba wanashiriki vyema katika shughuli za maendeleo yao ili
waweze kuondokana na baadhi ya kero zinazowakabili katika maisha yao ya kila
siku.
Aidha Mpenda amewakumbusha wakulima
kutumia mvua zilizoanza kunyesha msimu wa mwaka huu katika maeneo mbalimbali, wajikite
zaidi katika shughuli za kilimo badala ya kutumia muda wao mwingi kukaa vijiweni
na kuzungumzia mambo yanayoweza kuwarudisha nyuma kiuchumi.
Mpenda alitoa kauli hiyo juzi kwa
nyakati tofauti wakati alipokuwa akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya
maendeleo vijijini ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali
na wananchi katika vijiji mbalimbali.
Alisema kuwa licha ya Serikali kuamua
kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo, hata hivyo bado wananchi wanaowajibu
mkubwa kushiriki kikamilifu badala ya kuiachia peke yake ifanye kila
jambo hata lile ambalo halihitaji gharama kubwa.
“Ni lazima sasa wananchi nao wabadilike
kwa kushiriki kikamilifu katika kazi za kujitolea ikiwemo ujenzi wa zahanati na
mabweni katika maeneo yao, haiwezekani hata kidogo Serikali ndiyo ifanye
kila kitu hata yale yanayohitaji kufanywa na nguvu za wananchi”, alisema
Mpenda.
Alifafanua kuwa Serikali kupitia Halmashauri
ya wilaya ya Madaba imepanga kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu,
maji na ujenzi wa barabara kwa lengo la kuboresha na kusogeza huduma za kijamii
karibu na wananchi.
Vilevile aliongeza kuwa endapo wananchi
hawatakuwa tayari kuunga mkono juhudi hizo, Serikali haitaweza kutekeleza
miradi hiyo kwa wakati mmoja kutokana na ufinyu wa fedha.
Alisema licha ya fedha kuwa kidogo
inayopangwa katika bajeti kutoka katika vyanzo vyake vya mapato ya ndani na
zile zinazoletwa na Serikali kuu, halmashauri hiyo imejipanga kuhakikisha kila
mradi unakamilika kwa wakati ili kuleta tija kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Mpenda
amewataka watumishi wa halmashauri ya Madaba kufanya kazi kwa kujituma wakati
wote jambo ambalo ana imani kwamba likizingatiwa litasaidia kwa kiasi
kikubwa kutoa huduma bora kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment