Na Muhidin Amri,
Tunduru.
JUMLA ya akina mama 16 wamepoteza maisha
katika kipindi cha mwaka mmoja, kutoka Januari mwaka jana hadi kufikia Desemba mwaka
huu kutokana na matatizo mbalimbali wakati walipokuwa wakijifungua
wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.
Imefafanuliwa kuwa vifo hivyo vimesababishwa
na mimba kutunga nje ya mirija ya uzazi, kutokwa damu nyingi wakati wa
kujifungua na upungufu mkubwa wa damu kwa akina mama wanaokwenda kujifungua hospitali.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mratibu wa
huduma ya afya, uzazi na mtoto wilayani humo, Salome Namlia alipokuwa
akizungumza na mwandishi wetu Ofisini kwake.
Namlia alibainisha kuwa hadi kufikia mwezi
Oktoba mwaka huu wajawazito 10,714 sawa na asilimia 81 walihudhuria kliniki na
kwamba waliojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma walikuwa 8,852 sawa na
aslimiia 67.
Alisema kuwa wastani wa vifo vya
akina mama wajawazito wilayani hapa ni 124 kati ya 100,000 lakini bado juhudi
zinafanyika kuhakikisha kwamba idadi hiyo inapungua hadi kufikia 100 kwa
100,000.
Kadhalika katika halmashauri ya
wilaya ya Tunduru jumla ya vituo vinavyotoa huduma ya afya ya uzazi ni 61
na kwamba huduma ya kujifungulia vipo 60 ambapo hospitali ni tatu, vituo vya
afya vitano na zahanati 53.
Vilevile kutoka mwaka 2016 hadi
Novemba 2017 jumla ya watoto 10,354 walizaliwa ambapo kati ya hao watoto
waliozaliwa hai walikuwa 9,087 waliozaliwa pacha walikuwa 234 na watoto
waliozaliwa uzito pungufu walikuwa 1,033 ambao ni sawa na asilimia 12.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa wilaya
hiyo, Dokta Wendy Robert alisema huduma za uzazi wa mpango zinazotolewa katika
vituo vyote 65 vya kutolea huduma za afya katika halmashauri ya wilaya ya
Tunduru katika kipindi cha 2016/2017 jumla ya wateja 21,166 waliandikishwa na
kuanza kutumia njia mbalimbali za uzazi wa mpango.
Pia alieleza kuwa upimaji wa Virusi Vya
Ukimwi (VVU) ulifanyika katika vituo 62 vya kutolea huduma za afya kwa kila
mama mjamzito na kila anayehudhuria Kliniki na kwamba katika kipindi hicho
akina mama wajawazito 10,714 walipimwa.
Dokta Robert alisema kuwa kuanzia
mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu pia akina mama 3,027 walipimwa na 91
walikutwa na VVU hata hivyo changamoto kubwa iliyopo sasa ni uhaba wa watumishi
wenye taaluma hasa katika vituo vya afya na zahanati pamoja na mwitikio mdogo
wa wenza wao kwenda Kliniki kupima afya zao.
Katika kukabiliana na changamoto hizo,
halmashauri imeendelea kutenga fedha katika bajeti yake ya kila mwaka kwa ajili
ya kuajiri watumishi wenye taaluma ya afya na kufanya uhamasishaji wa kutoa
elimu kwa kuwahimiza akina mama wajawazito kuwahi kliniki mapema kupima afya
zao.
No comments:
Post a Comment