Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANAFUNZI sita wa kike wanaosoma
katika shule ya Sekondari Kiamili iliyopo kwenye kata ya Kigonsera Wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamekatisha masomo yao katika kipindi cha mwaka huu kutokana
na kuwa wajawazito.
Imeelezwa kuwa wanafunzi hao kidato
cha kwanza yupo mmoja, cha tatu mmoja na kidato cha nne walikuwa wa nne ambao
ilibidi wahitimu masomo yao baada ya kufanya mtihani wao wa mwisho.
Changamoto hiyo inasababishwa na
shule hiyo kukosa mabweni ya kulala wanafunzi, kutokana na watoto wengi
hutembea umbali mrefu kutoka majumbani kwao pale wanapokwenda shuleni
kuhudhuria vipindi vya masomo.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa shule hiyo,
Frank Kinunda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea
shule hiyo kwa ajili ya kujionea maendeleo mbalimbali.
Kinunda alifafanua kuwa shule hiyo
ambayo ina wanafunzi 800 wakiwemo wavulana 450 na wasichana 350 changamoto
kubwa wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa vyumba vya kulala watoto hao ili
waweze kukabiliana na tatizo hilo lisiweze kuendelea kutokea.
Shule hiyo ambayo ni ya kata ina
bweni moja tu la kulala wanafunzi wa kike ambapo pia halitoshelezi mahitaji na
kwamba halmashauri ya wilaya ya Mbinga, kwa kushirikiana na wananchi wa kata ya
Kigonsera wamejenga bweni lingine moja la kulala watoto hao ili kuweza
kukabiliana na hali hiyo.
Alibainisha kuwa wanafunzi wengine
ambao ni wavulana wanaoishi mbali na shule wamekuwa wakati mwingine
wakilazimika kuwalaza kwenye vyumba vya madarasa.
Kwa upande wake Kaimu Afisa mipango
wa wilaya hiyo, Zainabu Mfinanga alisema kuwa katika kukabiliana na tatizo hilo
wamekuwa wakihamasisha wananchi kujitolea kujenga mabweni ya kulala wanafunzi katika
shule mbalimbali za sekondari zilizopo wilayani humo na halmashauri imekuwa
ikichangia vifaa vya kiwandani katika kuweza kukamilisha ujenzi husika.
“Wananchi wanapaswa kuendelea
kujitolea, waandae benki tofari za kutosha ili ujenzi uweze kuwa rahisi na sisi
kama halmashauri tuweze kuendelea kutoa vifaa vya kiwandani”, alisema Mfinanga.
Hata hivyo halmashauri ya wilaya ya
Mbinga imeweza kuipatia shule ya sekondari Kiamili vifaa vya kiwandani ili
kuweza kukamilisha ujenzi wa bweni linguine ambalo linajengwa sasa ikiwemo
saruji mifuko 100, bati 220, nondo na gharama nyingine za kuweza kukamilisha
ujenzi huo.
No comments:
Post a Comment